
NAHODHA wa zamani wa Italia na mshindi wa Kombe la Dunia, Fabio Cannavaro amefutwa kazi katika klabu ya Dinamo Zagreb ikiwa ni miezi mitatu tu tangu aajiriwe, taarifa ya mabingwa hao wa Croatia imesema.
Cannavaro aliyeiongoza Italia kubeba ubingwa Kombe la Dunia 2006 na kushinda Tuzo ya Ballon d’Or, aliteuliwa na Dinamo mwishoni mwa Desemba mwaka jana.
“Cannavaro sio kocha wa kikosi cha kwanza cha Dinamo,” ilisema taarifa ya klabu hiyo.
Kocha huyo, anakuwa ni wa tatu kutemwa na Dinamo kwa msimu huu, huku akiwa ameiongoza timu hiyo katika mechi 14, zikiwamo 10 za Ligi Kuu ya Croatia wakipambana kutetea taji.
Cannavaro ameiongoza Dinamo kushinda mechi tano za ligi nchini humo, akipata sare mbili na kupoteza tatu akiiacha ikiwa nafasi ya tatu katika msimamo.
Dinamo ina kibarua cha kuchuana na vinara wa ligi hiyo kwa sasa, Hajduk Split iliyowazidi pointi nane kupitia mechi nane zilizosalia.
Kwa mujibu wa duru la kispoti kutoka Croatia zimeripoti kuwa, kipigo cha mabao 3-0 ilichopewa na Istra 1961 wikiendi ndio ilikuwa sababu ya kupigwa chini kabla ya leo kutangazwa kufutwa kazi.
Kwa sasa kikosi hicho kitakuwa chini ya kocha msaidizi, Sandro Perkovic.
Kabla ya kupewa kikosi hicho, Cannavaro mwenye umri wa miaka 51 alikuwa akiinoa Udinese inayoshiriki Ligi Kuu ya Italia, Serie A.
Kabla ya hapo ameshawahi kuzinoa klabu kadhaa zilizopo Mashariki na Kati na China, pia akiiifundisha timu ya taifa ya China mwaka 2019.
Msimu huu aliiduwaza AC Milan ya Italia katika mechi za awali za Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa kuichapa 2-1, lakini haikuisaidia kuendelea na michuano hiyo iliyopo hatua ya robo fainali kwa sasa.