
Canada imetangaza siku ya Jumatano, Machi 12, nia yake ya kupunguza vikwazo vyake vya kifedha dhidi ya Syria na kuteua balozi katika nchi hiyo, wakati serikali ya mpito huko Damascus inatafuta uungwaji mkono wa kimataifa.
Imechapishwa:
Dakika 2
Matangazo ya kibiashara
“Canada inathibitisha dhamira yake ya kuunga mkono mageuzi ya kisiasa yenye amani na shirikishi yanayoongozwa na Syria,” amesema mjumbe maalum wa Canada kwa Syria, Omar Alghabra, ili kuzuia nchi hiyo “kuingia kwenye machafuko na ukosefu wa utulivu.”
Vikwazo dhidi ya nchi hiyo vitapunguzwa “ili kuruhusu fedha zinazotumwa na baadhi ya benki nchini humo, kama vile Benki Kuu ya Syria,” imesema taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Canada.
Balozi wa Canada nchini Lebanoni Stefanie McCollum sasa atahudumu kama balozi asiye mkazi nchini Syria.
Canada, kama nchi nyingine nyingi, iliweka vikwazo vizito kwa serikali ya Rais wa zamani Bashar Al Assad na kwa sehemu kubwa za uchumi wa Syria wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyoanza mnamo mwaka 2011.
Tangu kuanguka kwa Assad mwezi Desemba mwaka jana, mamlaka mpya ya Syria imekuwa ikitoa wito wa kuondolewa kikamilifu kwa vikwazo hivi ili kufufua uchumi na kujenga upya nchi hiyo, iliyoharibiwa na miaka 14 ya vita vya wenyewe kwa wenyewe.
“Vikwazo hivi vimetumika kama chombo dhidi ya utawala wa Assad na kuondolewa kwao kutaruhusu utoaji wa misaada, kuunga mkono juhudi za maendeleo ya ndani na kuchangia katika ujenzi wa haraka wa Syria,” imesema taarifa hiyo.
Umoja wa Ulaya pia ulitangaza mwishoni mwa mwezi Februari kusitishwa kwa vikwazo vinavyolenga sekta muhimu za kiuchumi nchini Syria ili kusaidia ujenzi mpya na kuunga mkono kipindi cha mpito. Lakini hali bado ni tete.
Rais wa mpito Ahmed al-Sharaa, ambaye alikuwa anaongoza kundi la waislamu wenye itikadi kali la Sunni la Hayat Tahrir al-Sham (HTS) kabla ya kunyakua mamlaka mwezi Disemba, ameahidi kulinda dini na makabila madogo ya Syria, lakini karibu raia 1,400 wameuawa tangu Machi 6, kulingana na Shirika la Kufuatilia Haki za Kibinadamu la Syria (SOHR).
“Tunalaani vikali ukatili huu na tunatoa wito kwa mamlaka za mpito kuchukua hatua zote muhimu kukomesha ghasia,” Waziri wa Mambo ya Nje wa Canada amesema katika taarifa hiyo.
“Raia lazima walindwe, utu na haki za binadamu za makundi yote ya kidini na kikabila lazima ziheshimiwe, na wahusika wa vitendo hivi lazima wawajibishwe.”