
KIPA Patrick Munthary wa Mashujaa, ameweka wazi kuongeza ushindani wa kupambana kubaki ndani ya nafasi ya tatu kwa makipa wanaoongoza kwa kutoruhusu mabao kwenye Ligi Kuu (Clean Sheet).
Munthary ana clean sheet 12 hadi sasa, ikiwa moja pungufu na alizonazo Diarra wa Yanga, mwenye 13 anayemfukuzia Moussa Camara wa Simba anayeongoza akiwa na 15.
Akizungumza na Mwanaspoti, Munthary amesema kwa sasa anachoangalia ni kuendelea kusalia ndani ya tatu bora kwa makipa wanaofanya vizuri kwa msimu huu.
“Siwezi kusema nitampiku Camara au Diarra, lakini ninachotaka, ni kuendelea kubaki hapa nilipo, nisitoke zaidi ya hapa kwa sababu ndio malengo yangu lakini huku nikiendelea kutokufungwa,” amesema Munthary na kuongeza;
“Makipa wa kigeni ukweli wameongeza chachu kubwa ya ushindani katika Ligi yetu, hii sio vita kwangu bali inaniongezea ubora wa kupambana kila siku.”
Akizungumzia nafasi ya kucheza timu ya taifa, Taifa Stars, Munthary alisema jambo hilo litafika, lakini kwa sasa akili yake ameiweka kwa Mashujaa imalize vizuri.
“Suala la mimi kucheza timu ya Taifa naamini muda wake ukifika watanzania wataniona, napenda kuitumikia nchi yangu na nitafanya kwa moyo mmoja,” amesema Munthary.
Munthary ndiye kipa mzawa pekee msimu huu anaonyesha ushindani dhidi ya wageni.
Munthary kabla ya kuibukia katika Mashujaa alipita katika Akademi ya Shule ya Makongo, JKT Ruvu (Sasa JKT Tanzania) na Transit Camp.