
Kipa namba moja wa Simba, Moussa Camara huenda akarejea kwenye lango la timu hiyo dhidi ya Al Masry leo, baada ya kuonekana anaendelea vizuri katika uwanja wa mazoezi.
Camara amekuwa nje ya kikosi cha Simba tangu Februari 24, 2025 alipopata majeraha ya nyama za paja katika mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Azam FC.
Hadi sasa Camara amekosekana katika michezo minne iliyocheza Simba katika mashindano yote ambayo miwili ni ya Ligi Kuu na miwili ya Kombe la Shirikisho la CRDB ambayo walicheza na timu za Coastal Union, Dodoma Jiji, TMA na Big Man.
Akizungumzia hali ya kipa huyo kocha wa Simba, Fadlu Davids amesema wana uwezekano wa kumtumia Camara leo.
“Hadi sasa amekuwa akipiga hatua nzuri na amekuwa akiendelea vizuri na mazoezi. Amekuwa katika hatua za mwisho za mazoezi yake na tutafanya uamuzi wa mwisho kama atakuwa sawa kucheza dhidi ya mpinzani wetu,” amesema Fadlu.
Camara alijiunga na Wekundu wa Msimbazi msimu huu akitokea kwenye Klabu ya Horoya ya Guinea ambapo amekuwa na msimu mzuri ndani ya kikosi cha Simba kwani mpaka sasa amefanikiwa kulinda lango la Simba mara 15 bila kuruhusu nyavu zake kutikiswa.
Katika mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika, Camara alifanikiwa kuchecheza michezo yote sita ya hatua ya makundi huku akifanikiwa kuzuia nyavu zake kutikiswa katika michezo mitatu dhidi ya CS Sfaxien uliochezwa ugenini, SC Constantine uliochezwa nyumbani pamoja na ule wa Bravos do Maquis uliochezwa nyumbani.
Iwapo kama kipa huyu raia wa Guinea atarejea uwanjani atazidi kuimarisha safu ya ulinzi ya kikosi cha Simba ambayo itaendelea kumkosa beki, Che Malone ambaye amekuwa nje ya kikosi tangu alipopata majeraha ya goti kwenye mchezo dhidi ya Azam FC.
Simba itavaana na Al Masry leo Aprili 2, 2025 saa 1:00 usiku katika mchezo wa kwanza wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika wakati mchezo wa marudiano utachezwa Aprili 9, 2025 kwenye uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.