Baraza la Mahusiano ya Kiislamu Marekani (CAIR) limekaribisha wito wa Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis wa kufanywa uchunguzi ili kubaini kama utawala wa Kizayuni umefanya mauaji ya kimbari ya Wapalestina katika Ukanda wa Ghaza, lakini limesisitiza kuwa hauhitajiki uchunguzi na uthibitisho kwa jambo lililo dhahiri.
“Tunakaribisha msimamo sahihi wa Papa Francis na tunawahimiza wafuasi wake wautii wito huo, wachukue msimamo na kudai haki na uwajibikaji,” ameeleza Mkurugenzi Mkuu taifa wa CAIR, Nihad Awad, katika taarifa.
Awad amesisitiza kwamba, wito huo uliotolewa na kiongozi huyo wa Wakatoliki inapasa umjumuishe pia Rais wa Marekani Joe Biden, ambaye ni Mkatoliki mwaminifu.
Pamoja na hayo, Mkurugenzi Mkuu wa CAIR amesema, ingawa kauli hiyo iliyotolewa na Papa inakaribishwa “hakuna haja ya kuthibitisha au kuchunguza jambo lililo dhahiri”.

Amefafanua: “nchi nyingi za Umoja wa Mataifa na mashirika yenye mamlaka ya kimataifa yamefikia hitimisho kwamba Israel inafanya mauaji ya kimbari. Kinachotakiwa ni kuchukuliwa hatua za kukomesha mauaji hayo”.
Katika ujumbe alioweka kwenye X, Albanese amesema, anatumai kuwa Papa Francis atapata wakati wa kusoma ripoti mbili ambazo ameandika yeye mwaka huu, pamoja na ile ya Kamati ya Umoja wa Mataifa Kuhusu Matendo ya Israel, “inayojumuisha mashtaka ya mauaji ya kimbari”.
Ripota huyo wa UN ameongeza kuwa hata mwandishi maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki ya chakula ametoa ripoti inayoshutumu uwekaji watu na njaa na kuharibu mamlaka na uhuru wa chakula kama kitendo cha mauaji ya kimbari…/