
Dar es Salaam. Ripoti ya Ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere inaonyesha baadhi ya taasisi za umma nchini zinamiliki mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) iliyopatikana kwa gharama kubwa.
Baada ya ukaguzi taasisi hizo zimekutwa zikimiliki mifumo hiyo kwa gharama zilizozidi wastani wa kawaida. Katika tathmini ya gharama za mifumo iliyotengenezwa ndani (inhouse) kutoka kwa taasisi zilizotembelewa, iligundulika kulikuwa na mifumo minne iliyonunuliwa kwa gharama kubwa zaidi ikilinganishwa na mifumo mingine yote.
Kichere ameripoti kuwa miongoni mwa mifumo hiyo ni Mfumo wa Uhasibu Serikalini (Muse), uliotengenezwa na Wizara ya Fedha, ndiyo ulikuwa wa gharama kubwa zaidi, ambapo uliigharimu Serikali Sh8.8 bilioni.
“Uchambuzi zaidi ulionesha gharama ya wastani ya kupata mifumo kupitia njia ya utengenezaji wa ndani ilikuwa Sh459.4 milioni,” anasema Kichere kwenye ripoti zake za mwaka 2023/24 zilizowasilishwa bungeni wiki iliyopita.
Kichere amesema utaratibu huo unakiuka kifungu cha 1.9.2 cha Vigezo vya Mapitio ya Miradi ya Tehama ya Serikali ya mwaka 2014, ambacho kinazitaka taasisi za umma kununua mifumo kwa gharama zinazolingana na thamani ya soko. Katika muktadha huu, taasisi za umma zilitarajiwa kupata mifumo yenye ufanisi wa gharama na inayolingana na thamani ya soko.
Mfumo mwingine ni ule wa Uwekaji Alama Kielektroniki (e-MAS) kutoka Taasisi ya Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), iliyogharimu Sh5.3 bilioni, Mfumo wa Malipo ya Haraka Tanzania (TIPS) wa taasisi ya Benki Kuu uliogharimu Sh4.9 bilioni. Pamoja na Jukwaa la Tiketi Kielektroniki (ETP) kutoka Kituo cha Taifa cha Data Mtandao uliogharimu Sh4.5 bilioni.
Kwa ujumla, imeonekana kuwa mifumo ya Tehama iliyotolewa kwa makandarasi wa nje (outsourced) ilinunuliwa kwa gharama kubwa zaidi ikilinganishwa na ile ya ndani wakati gharama ya wastani kwa mifumo hiyo ya nje ilikuwa Sh1.3 bilioni.
Aidha, tathmini zaidi ya mifumo ya nje ilibaini kuwa Mfumo wa Mtandao wa Serikali (Gov-Net) katika Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), uliowekwa kama mfumo wa mtandao, ndiyo ulikuwa wa gharama kubwa zaidi kati ya mifumo yote ya nje, kwa kuwa uliigharimu serikali Sh41.7 bilioni.
Aidha ripoti imegundua kuna upungufu wa taarifa za gharama za kifedha za mifumo ya Tehama kutokana na taasisi hazikuwa zikituma taarifa kamili na sahihi za gharama za kifedha za mifumo ya Tehama kwenye Tovuti ya Huduma za Tehama za Serikali (Government ICT Services Portal) inayosimamiwa na Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA).
Vilevile, e-GA haikuhakikisha usahihi wa taarifa hizo za gharama zilizowasilishwa na taasisi hizo kuhusu mifumo ya Tehama ya serikali.
Aidha, ukaguzi ulibaini kuwa kati ya miradi 438 ya Tehama iliyosajiliwa hadi mwaka 2024 asilimia 82.4 haikuwa na taarifa kuhusu ada za leseni, asilimia 95.9 haikuwa na taarifa za gharama za upangishaji (hosting).
Asilimia 82.6 haikujumuisha taarifa za gharama za msaada wa kiufundi, pia asilimia 93.4 ya mifumo hiyo haikuwa na taarifa za gharama za matengenezo au uboreshaji.
Hali hii inahusishwa zaidi na ukosefu wa maelezo ya kina ya gharama katika Mfumo wa GISP unaosimamiwa na e-GA.
Mapendekezo
Kwa ujumla, CAG Kichere ameshauri Mamlaka ya Serikali Mtandao kurekebisha vigezo vya mapitio ya miradi ili kuweka mahitaji wazi ya utambuzi na makadirio ya gharama za muda mrefu na muda mfupi zinazohusiana na mifumo ya Tehama iliyotengenezwa ndani.
Aidha, kuhakikisha kuwa gharama zote za mifumo ya Tehama iliyowekwa katika taasisi za umma zinarekodiwa na kuripotiwa ipasavyo ili kutoa taarifa sahihi kuhusu hali ya kifedha ya kukamilika kwa mradi.
Kuboresha utendaji wa tathmini za mara kwa mara za mifumo iliyotengenezwa ndani ili kuhakikisha ufanisi wa gharama, Kujenga uwezo wa ndani katika ujuzi na maarifa ya utengenezaji, matengenezo na utoaji wa msaada kwa taasisi nyingine za umma kwa lengo la kuhakikisha ufanisi wa gharama katika mifumo ya Tehama iliyotengenezwa ndani.
“Kuhakikisha taasisi za umma zinashirikisha wadau muhimu katika hatua zote za maendeleo ya mifumo ya Tehama kuanzia hatua ya utengenezaji hadi utekelezaji wake,” ameshauri.