
Dar es Salaam. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere amebaini madeni ya mikopo yanayokabiliwa na hatari ya kutorejeshwa ya Sh2.58 bilioni katika Mfuko wa Maendeleo ya Vijana.
Katika aya ya 6.1 ya mwongozo wa Mfuko wa Maendeleo ya Vijana wa Mei 2022, inabainishwa kwamba kipindi cha kurejesha mikopo hakitazidi miezi 36 kuanzia tarehe mkopo ulipotolewa kwa vikundi vya vijana.
Hata hivyo, CAG amebaini kuwa kiasi hicho hakikulipwa kwa kipindi cha kati ya miaka mitatu hadi 21.
Hayo yamo katika Ripoti Kuu ya Mwaka ya Ukaguzi wa Serikali Kuu kwa mwaka wa fedha 2023/24 iliyotolewa bungeni Aprili 16, 2025, katika kipengele cha usimamizi wa mifuko maalumu na mingine.
“Mapitio yangu ya mfuko katika Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu (OWM-KVAU) yalibaini madeni ya mikopo yasiyolipwa yenye jumla ya Sh5.02 bilioni kutoka kwa mamlaka za Serikali za mitaa, ambazo zinawajibika kutoa mikopo kwa vijana, hadi Juni 30, 2024. Hasa, Sh2.58 bilioni, sawa na asilimia 51 ya kiasi hicho, kilikuwa hakijalipwa kwa kipindi cha kati ya miaka mitatu hadi 21,” amesema.
Amesema amehusisha udhaifu huo na kushindwa kwa menejimenti kufuatilia vyema mikopo iliyotolewa kwa mamlaka za Serikali za mitaa ili itolewe kwa vijana.
CAG amesema kushindwa kukusanya mikopo kutoka kwa vikundi vya vijana na watu binafsi kumekwamisha utoaji wa mikopo mipya kwa vikundi vingine vinavyohitaji, na hatimaye kukwamisha lengo la mfuko la kusaidia shughuli za kiuchumi za vijana na kupunguza ukosefu wa ajira.
“Napendekeza menejimenti ya OWM-KVAU ifanye ufuatiliaji na tathmini ya mara kwa mara ya mchakato wa utoaji mikopo na urejeshaji wake kwenye ngazi ya halmashauri.
“Aidha, hatua stahiki zichukuliwe dhidi ya wanufaika ili kurejesha mikopo ambayo haijalipwa kwa muda mrefu,” amependekeza.
Pamoja na hayo, CAG amebaini mikopo yenye thamani ya Sh1.28 bilioni ilitolewa kwa vikundi vya vijana kabla ya kupatiwa mafunzo na ushauri.
Amesema hiyo ni kinyume na aya ya 4.1.2 ya mwongozo wa Mfuko wa Maendeleo ya Vijana wa mwaka 2022, unaotaka wanufaika wa mikopo kufanyiwa mafunzo ya awali kuhusu huduma za maendeleo ya biashara, ujasiriamali na usimamizi wa kifedha kabla ya kutolewa kwa fedha.
CAG amesema Kamati ya Kiufundi ya Mfuko wa Maendeleo ya Vijana inaweza kushirikiana na wadau wengine au kuajiri wataalamu wa mafunzo inapohitajika. Mafunzo ya baada ya ufadhili na ushauri kwa wanufaika yatatolewa ili kuhakikisha uwezo wa vijana kurejesha mikopo na kufanya vizuri.
“Kinyume chake, ukaguzi wangu ulibaini kuwa katika mwaka wa fedha 2023/24, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu (OWM-KVAU) ilitoa mikopo yenye jumla ya Sh1.28 bilioni kupitia mfuko huo kabla ya wanufaika kupata mafunzo na ushauri muhimu,” amesema.
Kichere amesema anahusisha tatizo hilo na ukosefu wa ufuatiliaji na tathmini, kwani wizara ilishindwa kutekeleza shughuli hizo muhimu.
Ameshauri kuwa kutoa mikopo bila mafunzo ya maendeleo ya biashara kunaongeza hatari ya wanufaika kutosimamia vyema fedha hizo, na kufanya urejeshaji wa mikopo kuwa changamoto, jambo litakalosababisha kutofikiwa kwa malengo ya mfuko.
“Ninapendekeza menejimenti ya OWM-KVAU itoe mafunzo na ushauri kwa wanufaika wa mikopo kabla ya kutoa mikopo. Hii itachangia kujenga uwezo na kuimarisha ujuzi wa kibiashara kwa wanufaika.
“Pia, ihakikishe fedha hazitumiki kwa shughuli zilizo nje ya malengo ya mikopo husika. Vilevile, itoe kipaumbele kwenye ufuatiliaji na tathmini,” amesema.