
Dodoma. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere ameomba mkutano wa 19 wa Bunge unaoendelea utenge muda wa kujadili ripoti yake kwa mwaka wa fedha 2023/24 iliyowasilishwa mapema bungeni leo Jumatano, Aprili 16, 2025.
Kichere ametoa ombi hilo leo Jumatano April 16, 2025 alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma wakati akitoa ufafanuzi wa ripoti yake kwa mwaka 2023/24 huku akitoa sababu za ombi hilo kuwa, huu ni mkutano wa mwisho kabla ya wabunge kuelekea kwenye uchaguzi mkuu hivyo hakutakuwa na muda wa kuijadili.
Kanuni za Bunge zinaelekeza, ripoti za CAG zinapaswa kujadiliwa bungeni katika mkutano wa tatu wa Bunge wa kila mwaka ambao hufanyika mwezi Septemba.
Hata hivyo, Rais Samia Suluhu Hassan anatarajia kulihutubia Bunge Juni 27, 2025 ambapo hotuba yake itatamka kulivunja Bunge la 12 hivyo Septemba hakutakuwa na mkutano mwingine hadi baada ya uchaguzi Mkuu.
“Hata mimi naona ikiwapendeza basi taarifa hizi zijadiliwe hapa katikati wakati mkutano huu ukiendelea kwani sote tunaamini baada ya hapa hakutakuwa na Bunge hadi uchaguzi mkuu utakapofanyika na hivyo nafasi ya kujadili haitakuwepo tena,” amesema Kichere.
CAG amesema wako kwenye mazungumzo ili kuona namna gani ripoti hizo zitakuwa zikijadiliwa ndani ya Bunge zikiwa bado za moto kuliko kusubiri wakati mwingine muda unakuwa umepita zaidi.
“Zamani ilichukua karibu mwaka ndipo wajadili, lakini wakasogeza kidogo na sasa tunataka wasogeze zaidi maana mchuzi wa mbwa unanywewa ungali wa moto bado,” amesema Kichere.
Akijibu maswali ya waandishi amekiri wakati mwingine taasisi au mashirika yanaweza kupata hati safi lakini ndani yake kukawa na changamoto hivyo wanafanya kazi kwa weledi mkubwa ili kubaini mapungufu ya namna hiyo.
Amesisitiza inampa wakati mgumu kuona mashirika yaliyoanzishwa kibiashara nayo yanakuwa na hasara wakati yalipaswa kupata faida hivyo akasema baadhi wanaweza kuwa na hati safi lakini ndani yake kukawa na changamoto.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), Halima Mdee amesema bado kuna maeneo yanashida licha ya taasisi nyingi kupata hati safi na kujiona kama wamefanikiwa.
Mdee amesema taasisi zilizochini ya LAAC zote 220 zilipata hati zinazoridhisha lakini akashauri ipo haja ya kujiridhisha zaidi kama fedha za wananchi zinatumika kama inavyotakiwa kwani baadhi ya maeneo fedha zinaonekana kwenye mitandao tu.
“Eneo la miradi ya maendeleo huko bado kuna tatizo kubwa, fedha ambazo Bunge tulipitishwa ni nyingi lakini zaidi ya 1125 bilioni zilirudishwa Hazina hebu tuangalie hapo kuna kitu gani,” amesema Mdee.
Mbunge huyo amesisitiza Watanzania kuisoma taarifa ya CAG katika maeneo yote 14 ili wapate ufahamu wa namna gani wanaweza kutambua rasilimali zao zinavyopotea.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge, Oran Njeza amesema utaratibu mzuri utakaowezesha mapato ya Serikali kutokupotea hovyo, ni kwamba fedha zote lazima zipitie kwenye mfuko mkuu kwani bila kufanya hivyo tatizo bado lipo.
Njeza amemtaka CAG kuongeza makali katika ukaguzi akisema yeye (CAG) ndiyo jicho la Watanzania na kwamba hakuna anayeweza kusimama kama siyo mtaalamu huyo na kikosi kizima cha ukaguzi.