
Dar es Salaam. Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) inaonyesha kuwa ni Watanzania watatu kati ya 10 pekee ndio wamesajiliwa na kupewa vyeti vya kuzaliwa, huku saba wakiwa hawana taarifa za kuzaliwa zao.
Ripoti hiyo ya mwaka 2023/24, iliyojikita katika kuangazia utambulisho, usajili, na utoaji wa vyeti vya kuzaliwa na vifo, inaonesha kuwa ni asilimia 29 pekee ya watu wa Tanzania Bara ndio wamesajiliwa na wana vyeti vya kuzaliwa
Ripoti hiyo ya CAG inaonesha kuwa, hadi Desemba 2024, Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita) imesajili watu 18,464,255 kati ya 63,743,121 wanaokadiriwa kuzaliwa Tanzania Bara.
hiyo inabaini kwamba idadi ndogo ya waliosajiliwa inasababisha wananchi kutafuta vyeti wakati vinahitajika kwa shughuli za elimu, ajira, na nyingine.
Ripoti pia inaonyesha kuwa Rita ilikosa kufikia lengo la usajili wa vyeti vya kuzaliwa katika kipindi cha miaka mitatu, ambapo ilikusanya vyeti 4,255,151 wakati lengo lilikuwa 4,903,962. Ikiendelea kwa kasi hii, itachukua miaka 27 kusajili watu 45,278,866 waliosalia.
Ukaguzi pia umebaini ucheleweshwaji wa uchakataji wa maombi ya vyeti vya kuzaliwa, ambapo baadhi ya maombi yanachukua hadi siku 557 badala ya tano kama inavyotakiwa.
Pia, ripoti inaonyesha ucheleweshwaji katika usajili wa vifo, ambapo katika miaka mitatu, Rita ilikusanya vifo 102,093, sawa na asilimia 39 ya lengo la usajili wa vifo 255,411.
Ucheleweshwaji huu unatokana na uhaba wa rasilimali watu, utegemezi wa mifumo ya maandishi kwa mkono, na makosa kwenye nyaraka.
CAG amependekeza Rita kufanya utafiti wa kina kubaini idadi halisi ya watu ambao hawajasajiliwa na kutoa vyeti vya kuzaliwa, na kuweka rasilimali za kutosha kuhakikisha usajili na utoaji wa vyeti unafanyika kwa wakati.