
Arusha. Taasisi 24 za umma kati ya 78 hazikuwa na mikataba rasmi wala makubaliano ya viwango na watoa huduma wao wa mifumo ya Teknolojia za Habari na Mawasiliano (Tehama), hali iliyosababisha ukosefu wa uwajibikaji na kushusha viwango vya ubora wa huduma zilizotolewa na watoa huduma wa nje.
Hayo yamebainika baada ya ukaguzi uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere katika mwaka wa fedha 2023/24 wakati wa ukaguzi wa mifumo ya Tehama.
Ukaguzi huo kwenye taasisi hizo 78 ulijumuisha mifumo minne mikuu ya Serikali inayotumika katika usimamizi wa fedha za umma na utoaji huduma.
Mifumo hiyo ni wa Uhasibu Serikalini (Muse), Mfumo wa Usimamizi wa Bajeti Kuu (Cbms), Mfumo wa Usimamizi wa Mali za Serikali (Gamis) na Mfumo wa Malipo ya Kielektroniki wa Serikali na Mfumo wa Usimamizi wa Rasilimali-watu (Gepg &Hcmis).
Ripoti hiyo imeainisha usimamizi wa hatari zinazotokana na watoa huduma wa nje ni muhimu katika kuhakikisha ubora wa huduma, uwajibikaji na usalama wa taarifa.
CAG amesema ukaguzi umebaini upungufu katika usimamizi wa watoa huduma, hali ambayo ingeziweka taasisi katika hatari ya kushuka kwa ubora wa huduma, kukosekana kwa uwajibikaji na athari za kiusalama kwa mifumo ya Tehama.
“Taasisi 24 kati ya 78 hazikuwa na mikataba rasmi wala makubaliano ya viwango vya huduma na watoa huduma wao wa Tehama, na kukosekana kwa mikataba rasmi kulisababisha ukosefu wa uwajibikaji na kushusha viwango vya ubora wa huduma zilizotolewa na watoa huduma wa nje,” amesema CAG Kichere.
Ripoti imesema taasisi 62 hazikufuatilia ufanisi wa utendaji wa watoa huduma, jambo lililohatarisha uzingatiaji wa masharti ya mikataba na kupunguza ubora wa huduma zilizotolewa.
“Ukaguzi pia ulibaini katika baadhi ya taasisi, watoahuduma walipewa haki zisizodhibitiwa za kuingia kwenye miundombinu muhimu ya Tehama, hali ambayo ingeleta hatari za kiusalama na kiutendaji,” amesema.
Ripoti hiyo ya CAG, imetolea mfano katika tukio moja, mtoa huduma aliendelea kuwa na haki za kuingia kwenye seva na hifadhi data ya mfumo licha ya kulazimika kukabidhi rasmi haki hizo kwa taasisi ndani ya muda uliokubaliwa.
Katika tukio jingine, mtoa huduma alikuwa na haki ya kuingia na kutumia hifadhi data ya mfumo, hali ambayo ilizuia watumishi wa Tehama wa taasisi husika kufanya usimamizi wa mfumo huo.
“Upungufu huu ulitokana na usimamizi hafifu wa mikataba ya watoa huduma na kutotekelezwa kwa taratibu za udhibiti wa haki za upatikanaji wa mifumo, hali ambayo ingeweza kusababisha athari kubwa kama vile matumizi mabaya ya taarifa, marekebisho yasiyoidhinishwa ya mifumo na utegemezi mkubwa wa taasisi kwa watoa huduma wa nje,” amesema.
CAG amependekeza kuandaliwa mikataba na makubaliano rasmi ya viwango vya huduma katika kila taasisi, kufuatilia utendaji wa watoa huduma ili kuhakikisha wanatoa huduma kwa viwango vinavyotarajiwa.
“Taasisi zihakikishe upatikanaji wa hifadhi data kwa watoa huduma unadhibitiwa kikamilifu na unatolewa pale inapohitajika tu, pia akaunti zilizo na ruhusa za kufikia seva na hifadhi data zipitiwe mara kwa mara ili kuimarisha usalama wa mifumo na uhuru wa taasisi katika kuendesha mifumo yao,” amesema.
Mwendelezo wa huduma
Ukaguzi huo ulilenga kutathmini utayari wa taasisi na mbinu za usimamizi zinazohusiana na mipango ya mwendelezo wa huduma na mahusiano na watoa huduma katika taasisi hizo 78 ambapo ilibaini upungufu mkubwa katika utayari wa taasisi kujilinda na majanga ya Tehama na usimamizi wa watoa huduma.
CAG amesema upungufu huo ulizua hatari zinazoweza kuathiri kwa kiasi kikubwa shughuli za taasisi endapo hazitashughulikiwa ipasavyo.
Amesema kati ya taasisi 78, taasisi 23 hazikuwa na mipango ya mwendelezo wa shughuli (BCP) au mipango ya urejeshaji wa huduma baada ya majanga (DRP), hali iliyozua wasiwasi mkubwa kuhusu uwezo wa taasisi hizo kukabiliana na usumbufu kwa shughuli zao wakati wa matukio yasiyotarajiwa.
“Aidha taasisi 55 hazikufanya majaribio ya mara kwa mara ya mipango yao ya mwendelezo wa shughuli na urejeshaji wa huduma, hatua ambayo ni muhimu katika kuhakiki ufanisi wa mipango hiyo na kuhakikisha taasisi ziko tayari kukabiliana na changamoto za dharura,” amesema.
Amesema kukosekana kwa majaribio haya kulipunguza uwezo wa taasisi kudhibiti athari za majanga na mabadiliko makubwa ya kiutendaji.
CAG amependekeza taasisi kuandaa na kuweka nyaraka rasmi za mipango ya mwendelezo wa shughuli na mipango ya urejeshaji wa huduma ili kuimarisha utayari wa kukabiliana na hali za dharura, na kufanya majaribio ya mara kwa mara ili kuthibitisha ufanisi wake na kuhakikisha kuwa mipango hiyo inakidhi mahitaji ya taasisi.
Wakati ripoti ya CAG ikibaini hayo, Aprili 10, 2025 jijini Arusha, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Tehama (ICTC), Dk Nkundwe Mwasaga, alisema Tanzania imeendelea kujiimarisha na kuongeza nguvu kwenye usalama mtandao ili kukuza uchumi wa kidijitali pamoja na kuvutia wawekezaji.
Amesema kupitia Shirika la Mawasiliano Duniani (ITU), Tanzania imekuwa miongoni mwa nchi 47 bora zilizowekwa kwenye kundi la kwanza zenye mitandao bora salama.
Akizungumza katika Jukwaa la nne la usalama wa mtandao lililokutanisha wataalamu wa Tehama wa ndani na nje ya nchi, amesema katika uchumi wa kidijitali, huduma nyingi zinatolewa kwa kutumia mitandao hivyo wanawaangalia walaji kwa makini.
“Tunatumia wataalamu kuhakikisha mifumo yetu inakuwa madhubuti kwani jambo mojawapo linalovutia wawekezaji wa kidijitali ni usalama mtandaoni,” alisema.
“Ukiangalia mkakati wetu wa mapinduzi ya kidijitali una nguzo tano ikiwemo usalama mitandao, ulinzi wa taarifa binafsi na kumlinda mlaji, katika masuala haya yote tunamuangalia mlaji (mtumiaji wa mwisho) aweze kupata huduma vizuri,”amesema