
Dar es Salaam. Fidia kwa watu walioathiriwa na miradi (PAPs) zenye thamani ya Sh27.81 bilioni katika miradi mitatu ya miundombinu ya barabara na mmoja wa maji haikulipwa, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere amebaini.
Imebainika fidia hizo hazikulipwa licha ya kuendelea kutekelezwa kwa miradi hiyo, na kupita kwa muda wa ripoti za tathImini.
Hayo yamo katika Ripoti ya Ukaguzi ya Serikali Kuu kwa mwaka wa fedha 2023/24 iliyowasilishwa Bungeni leo Jumatano, Aprili 16, 2025 na CAG kuhusu usimamizi wa ununuzi.
CAG amesema kanuni ya 13 (1-3) ya kanuni ya ardhi (tathmini ya thamani ya ardhi kwa ajili ya fidia) ya mwaka 2001 inataka kiasi ambacho kitalipwa kama fidia kiwe cha haki, cha kutosha na kilipwe kwa wakati ndani ya miezi sita kuanzia tarehe ya uthamini.
Vinginevyo, riba ya kiwango kinachotolewa na benki za biashara kwenye amana za kudumu, kitatozwa hadi fidia hizo zitakapolipwa.
“Nilibaini kuwa fidia kwa watu walioathiriwa na miradi (PAPs) zenye jumla ya Sh27.81 bilioni kwa miradi mitatu ya miundombinu ya barabara na mmoja wa maji, haikulipwa licha kuendelea kutekelezwa kwa miradi hiyo na kupita kwa muda wa ripoti za tathImini,” amesema na kuongeza.
“Wakati wa ukaguzi wa miundombinu ya barabara, nilibaini kwamba fidia ya Sh1.21 bilioni haikulipwa kwa waathirika na miradi (PAPs) kwa Mradi wa Barabara ya Same–Kisiwani–Mkomazi hadi Novemba 2024, licha ya ripoti ya tathImini kuwa imepitwa na muda wa miezi sita,” amesema.
Vilevile, amesema fidia ya jumla ya Sh5.52 bilioni haikulipwa kwa waathirika 1,799 kwenye mradi wa barabara ya Sabasaba–Sepuka–Ndago–Kitaza, pamoja na Sh13.5 bilioni haikulipwa kwa waathirika 1,256 kwenye miradi mbalimbali ya miundombinu ya barabara za Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads).
Amesema Tanroads pia ilikuwa na deni la Sh6.61 bilioni ambalo ni fidia kwa wamiliki wa ardhi hadi Septemba 2024, ambapo fedha hizo zilikuwa zimeombwa kutoka Wizara ya Fedha tangu Desemba 2023, lakini hazikutolewa.
Amesema wakati wa utekelezaji wa mradi wa kusambaza maji katika vijiji 27 katika Wilaya za Muheza, Handeni na Mji wa Korogwe alibaini kuwa watu 554 walioathiriwa na mradi (PAPs), pamoja na Chama cha Ushirika wa Kilimo na Masoko cha Mgombezi hawajalipwa fidia ya jumla ya Sh971.47 milioni, licha ya mradi kufikia asilimia 60 ya utekelezaji.
Ucheleweshaji huo wa malipo ya fidia unachangiwa na kuchelewa kutolewa kwa fedha kutoka Wizara ya Fedha.
Amesema kuchelewa kwa fidia hizo kunaweza kusababisha kutozwa kwa riba au kufanya tathimini upya ili kuendana na kiwango cha malipo ya fidia, pia kunaweza kusababisha kuchelewa kwa utekelezaji wa miradi na inaweza kuleta ongezeko la gharama.
“Ninapendekeza Serikali ihakikishe kuwa Wizara ya Fedha inatoa fedha za fidia kwa wakati ili kuepuka malimbikizo ya riba na uhitaji wa kufanya tathmini upya kwa watu waliathiriwa na miradi,” amesema Kichere.