
Dar es Salaam. Mamlaka za serikali za mitaa 42, sekretarieti za mikoa mbili zimechepusha Sh13.99 bilioni ili kugharamia shughuli nyingine za maendeleo na matumizi ya kawaida.
Mbali na mamlaka hizo, pia Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart), ulitumia Sh2.04 bilioni zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya fidia na mfuko wa usafiri wa abiria kwa shughuli nyingine zisizokusudiwa.
Uchepushaji huo wa fedha umebainishwa katika Ripoti ya mwaka ya ukaguzi wa Tamisemi, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa wa mwaka wa fedha 2023/24 ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
CAG, Charles Kichere amesema hatua hiyo ya fedha kutumika kinyume na bajeti na kuathiri utekelezaji wa shughuli zilizopangwa.
Kuhusu Dart, Kichere amesema: “Hii ni kinyume na kanuni ya 5.2.1 (d) ya Dart ya mwaka 2014 ambayo inamtaka mtendaji mkuu wa wakala kuhakikisha kuwa fedha zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na masharti yote yanayohusiana na fedha hizo yanazingatiwa.”
Kichere amesema hadi Juni 30, 2024 ilibaki Sh1.8 milioni wakati madai ya fidia yalikuwa ni Sh1.94 bilioni.
“Jumla ya Sh16.03 bilioni zilichepushwa na Dart, sekretarieti za mikoa na mamlaka za serikali za mitaa katika mwaka wa fedha 2023/24, ikiwa ni ongezeko la Sh3.20 bilioni ikilinganishwa na Sh12.83 bilioni zilizochepushwa mwaka wa fedha 2022/23,”amesema.
“Hali hii inaonesha kuna mwendelezo wa uchepushaji wa fedha, ambapo zinatumika kinyume na bajeti iliyopangwa,” amesema Kichere katika ripoti hiyo iliyowasilishwa leo Jumatano, Aprili 16, 2025 bungeni jijini Dodoma.
Athari za uchepushaji fedha
Kutokana na hilo, Kichere amesema uchepushwaji wa fedha unaweza kuathiri utoaji wa huduma kwa jamii, kwa miradi iliyokusudiwa kutotekelezwa au kusababisha utekelezaji miradi isiyo na manufaa kwa jamii.
Njia za kuzuia uchepushaji
Kichere amesema ili kuzuia uchepushaji fedha na kuhakikisha utoaji wa huduma bora, Wizara ya Fedha na mamlaka husika zinapaswa kuimarisha ufuatiliaji wa bajeti, kusimamia utekelezaji madhubuti wa kanuni za fedha, na kuongeza uwazi katika matumizi ya fedha.
“Vilevile, mabadiliko yote ya bajeti yanapaswa kupitishwa kwa taratibu sahihi za kibajeti, kwa kuzingatia utoaji wa fedha kwenye miradi inayotekelezeka na inayokidhi mahitaji ya jamii,” ameshauri Kichere.