
Dar es Salaam. Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limeufungia kwa muda Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam kutokana na eneo la kuchezea (pitch) kuendelea kupungua ubora wake.
CAF imeelekeza eneo hilo liboreshwe haraka kufikia viwango vinavyotakiwa ili kuepuka uwanja huo kufungiwa kwa muda mrefu.
Katika taarifa iliyotolewa leo Jumatano Machi 12, 2025 na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imeeleza kuwa kutokana na hatua hiyo mechi ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho la CAF (CAFCC) kati ya Simba na Al Masry ya Misri iliyopangwa kuchezewa uwanjani hapo Aprili 9 ipangiwe eneo lingine.
“Ili kuondoa usumbufu, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limetakiwa kutuma jina la uwanja mbadala utakaotumiwa na Simba kufikia Machi 14, 2025.
“CAF itafanya ukaguzi wa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Machi 20, 2025 ili kuona maboresho yaliyofanyika kabla ya kuamua kuuruhusu utumike au kuendelea kuufungia,”imeeleza taarifa hiyo.
Awali, mbali na mechi za shirikisho, pia Uwanja wa Benjamin Mkapa umepangwa kutumika kwa ajili ya fanali za mataifa ya afrika kwa wachezaji wa ligi za ndani (CHAN) zitakazofanyika Agosti 2025.
Kufungiwa kwa Uwanja wa Benjamin Mkapa ni pigo la pili kwa Simba kwenye mashindano hayo msimu huu kwani la kwanza lilikuwa ni kupata adhabu ya kucheza bila mashabiki katika mechi ya mwisho ya hatua ya makundi dhidi ya CS Constantine ya Algeria, Januari 19, 2025.
Katika mchezo huo, Simba iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 yaliyoifanya iongoze kundi A la mashindano hayo.