Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) imetoa adhabu kali kwa timu za MC Alger na Esperance kutokana na vurugu za mashabiki, wachezaji na maofisa wao ugenini katika mechi za hatua ya robo fainali dhidi ya Orlando Pirates na Mamelodi Sundowns.

Kamati ya nidhamu ya CAF, imeitoza MC Alger faini ya fedha kiasi cha Dola 100,000 (Sh269 milioni) kwa kosa la vurugu ambazo timu na mashabiki wake walifanya dhidi ya Orlando Pirates kwenye Uwanja wa Orlando, Johannesburg, Aprili 9 mwaka huu.

Kocha msaidizi wa MC Alger, Mohamed Khezrouni amepewa adhabu ya kufungiwa michezo minne ya CAF huku beki wake Abdelkader Oussama Menezia akifungiwa mechi mbili.
Esperance nayo imetozwa kiasi cha Dola 100,000 kwa kosa la vurugu ambazo mashabiki wake walifanya Aprili Mosi mwaka huu dhidi ya Mamelodi Sundowns katika Uwanja wa Loftus Versfeld.

Katika mchezo huo, Mamelodi Sundowns iliibuka na ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na Peter Shalulile.
Mamelodi Sundowns ilifanikiwa kusonga mbele kwa ushindi wa bao 1-0 kwani mechi ya marudiano Tunisia, timu hizo zilitoka sare tasa.

Orlando Pirates nayo ilitoka sare ya bila kufungana katika mechi hiyo ya Aprili 9 nyumbani lakini ikasonga mbele kwa vile iliibuka na ushindi wa bao 1-0 ugenini, Aprili Mosi.