Dar es Salaam. Baada ya Ivory Coast kutangaza kujitoa kuandaa fainali za Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 20 (AFCON U20), Shirikisho la Mpira wa Miguu Misri (EFA) limezawadiwa haki ya kuandaa mashindano hayo.
Timu ya taifa ya vijana ya Tanzania chini ya umri wa miaka 20 ‘Ngorongoro Heroes’ ni miongoni mwa timu zitakazoshiriki mashindano hayo.
Taarifa iliyotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) jana Machi 27, 2025, imefafanua kuwa shirikisho hilo limeamua hivyo kwa vile Misri imeonyesha utayari na iliwahi kuomba kuandaa mashindano hayo.
“Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) leo (jana) limekabidhi Shirikisho la Soka la Misri (EFA) na Serikali ya Misri haki ya kuandaa Kombe la Mataifa ya Afrika la Vijana chini ya umri wa miaka 20, 2025.

“Hii ni baada ya CAF kufahamishwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Ivory Coast (FIF) na Serikali ya Ivory Coast kwamba kutokana na hali zisizotarajiwa, hawawezi kuandaa michuano hiyo.
“Shirikisho la Soka la Misri na Serikali ya Misri hapo awali waliwasilisha ombi la kuandaa Kombe la Mataifa ya Afrika la Vijana chini ya umri wa miaka 20, 2025. Mechi ya ufunguzi ya Kombe la Mataifa ya Afrika la Vijana chini ya miaka 20, 2025 itachezwa Jumapili, Aprili 27, 2025 na Fainali mnamo Mei 18, 2025,” imefafanua taarifa ya CAF.

Fainali za Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 20, zinashirikisha idadi ya timu 12 zilizogawanywa katika makundi matatu yenye timu nne kila moja.
Timu hizo 12 zinazoshiriki Afcon U20 mwaka huu ni Morocco, Zambia, Tanzania, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Senegal, Sierra Leone, Ghana, Nigeria, DR Congo, Kenya na Afrika Kusini.
Hii ni mara ya pili kwa Ngorongoro Heroes kushiriki fainali za AFCON U20 ambapo mara ya kwanza ilikuwa ni 2021 pindi yalipofanyika Mauriatania ambapo timu hiyo iliishia katika hatua ya makundi.
Katika fainali za AFCON U20 mwaka huu, Ngorongoro Heroes imepangwa kwenye kundi A na timu za DR Congo, Jamhuri ya Afrika ya Kati na Ghana.
Timu nne zitakazoingia nusu fainali kwenye fainali za AFCON U20 2025 zitafuzu Fainali za Kombe la Dunia kwa vijana wa umri huo zitakazofanyika Chile baadaye mwaka huu.