Cadabra Bondia bishoo anayeutaka mkanda wa WBO

Majina makubwa Kinondoni katika upande wa burudani basi katu huwezi kuliacha jina la mkongwe wa Bongo Fleva, Top in Dar ingawa wengi wanamtambua kama TID lakini kabla ya kujiita Kigogo.

Ni ngumu sana kuitaja Kino bila ya kuhusisha jina lake kama sasa ilivyo kwa Bilnass ambaye amekuwa akipasua kwenye mziki wa Bongo Fleva kwa kuendelea kutoa ngoma kali kila uchwao.

Lakini kwenye upande wa michezo basi kwenye soka litakuja jina la kiungo wa zamani wa Simba na sasa Yanga, Jonas Mkude ‘Nungunungu’ ila kwenye mchezo wangu basi huwezi kuliacha jina la Francis Miyeyusho ‘Chichi Mawe’ huyu alipiga ile familia ya Matumla, baba na mtoto.

Katika jiji la Dar, Kinondoni wanasifika kwa mabishoo ‘Brother Man’ wengi ndiyo anapotokea bondia chipukizi katika mchezo wa ngumi za kulipwa nchini, Abdada Ferouz ‘Cadabra’ kutoka Mafia Boxing Gym.

Siyo rahisi kwa Wazungu kukubali kama huna uwezo wowote lakini kwa Cadabra imekuwa totauti  kwani wanaoundesha mtandao boxrec ambao ndiyo unahusika kuhifadhi taarifa za mabondia, wanakubali uwezo wake kutokana na kumpa asilimia mia za kupiga wapinzani kwa Knockout bila ya shida.

Bondia huyo mwenye rekodi ya kucheza mapambano manne pekee ambayo yote amecheza mwaka jana akiwa chini ya Mafia Boxing Gym ambayo kwa sasa imekuwa nguzo kubwa ya mchezo huo nchini kutokana na kuandaa mapambano ya mara kwa mara yenye sura ya kitaifa.

Cadabra ambaye pambano lake kwanza alicheza Agosti 10, mwaka jana kwa kumchapa kwa Technical Knockout ya raundi ya kwanza Abdallah Mngola katika pambano la raundi sita kisha Oktoba 5 akamchakaza Waziri Magombana kwa Technical Knockout ya raundi tano katika pambano la raundi sita.

Novemba 16, akamchakaza kwa Technical Knockout ya raundi sita, Snowden Munyanje kutoka Malawi katika pambano la raundi nane kabla ya Desemba 26, katika pambano la Knockout ya Mama kumtwanga Latibu Muwonge wa Uganda kwa Technical Knockout ya raundi ya nne katika pambano la raundi nane.

Bondia huyo kwa sasa anakamata nafasi ya kwanza katika 57 mabondia bora wa uzani wa walter wakati duniani akiwa 140 katika mabondia 2224 huku akiwa amepewa hadhi ya nyota mbili na nusu.

Katika mahojiano yake na Mwananchi, Cadabra anasimulia kuwa jambo ambalo watu wengi hawalijui kuwa yeye alianza kucheza ngumi za ridhaa za mwaka 2017 hadi 2023 huku akipita katika klabu kubwa ya Ngome iliyopo chini ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania JWTZ ambayo inashikilia mabondia wengi wa kubwa kama Seleman Kidunda, George Bonabucha, Haruna Swanga na Ismail Galiatano.

“Unajua nimeanza kwenye ngumi za ridhaa ambazo nimecheza kwa muda mrefu toka 2017 nilipokuwa kwenye klabu Ngome lakini baadae nikaenda JKT Mgulani na nimeshiriki karibu mashindano mengi makubwa ya ngumi za ridhaa.

“Lakini kilichonifanya niingie kucheza ngumi zakulipwa, nadhani ni ugumu wa maisha na familia ambayo nimetokea, vimechangia mimi kuwa hapa leo.

Nani alikushawishi kuingia kwenye ngumi za kulipwa?

‘Nadhani sehemu kubwa ni watu ambao wamenizunguka kwa sababu nilitoka Kinondoni kwenda kuishi Manzese sasa kule nikakutana na bondia Adam Mbega, Emmanuel Amosi na Innocent, wao wmekuwa chachu kubwa kwangu kuingia kucheza ngumi za kulipwa.

“Nashukuru Mungu nimekuwa nikifanya vizuri tangu niingie kwenye ngumi za kulipwa, matokeo yangu ya ushindi imekuwa ni Knockout jambo ambalo nifaraja kwangu pamoja na menejimenti yangu ya Mafua Boxing Gym ambayo imekuwa ikinisimamia.

Umejiunga vipi na Mafia?

“Nilianza kucheza Ngome halafu nikaenda JKT Mgulani baada ya kutoka hapo nikaenda timu ya Polisi kabla ya kurejea tena JKT Mgulani ambapo ndiyo Mafia waliniona na kunichukua kutokana na kuvutiwa na uwezo wangu ambao nilionyesha kwenye mashindano ya ngumi za ridhaa.

“Mapambano yangu yote mpaka sasa nimecheza nikiwa chini ya Mafia na jambo kubwa ni kwamba sijawahi kupoteza pambano lolote tangu niingie kwenye ngumi za kulipwa.

Mipango yako ipo katika mchezo huu?

“Kiukweli kitu pekee ambacho nakilenga ni kuona nafika mbali kwa kuweza kucheza mapambano makubwa yenye mikanda mikubwa ambayo ndiyo msingi wa ngumi.

“Nataka kuona nafikia ndoto kushinda mikanda mikubwa ya ubingwa wa dunia kama WBC, WBO, IBO na IBF ambayo imekuwa sehemu muhimu na ndoto ya mabondia wengi duniani.

Kwanini unajiita bondia bishoo?

“Kwanza kabisa mimi sijiiti bisho ila mashabiki ndiyo wamekuwa wakiniita bishoo kwa sababu ya utanashati wangu ulivyo ndiyo imekuwa sababu kubwa ya kuitwa hivyo.

“Lakini naweza kusema kweli mimi ni bishoo haswaa kwa sababu hata muonekano wangu pia unaruhusu kuitwa bishoo maana nina vuto ila hata mtu ambaye amekuwa ‘role Model’ wangu ni bishoo sana.

“Nimekuwa nikimfuatilia na kumuangalia kama kioo, Ben Whittaker  ambaye ukimuangalia kawaida unaweza kusema mwepesi lakini akiwa kwenye ulingo anakuwa moto wa kuotea mbali ndiyo mimi nilivyo.

“Lakini mwisho wa yote bado nitoa shukrani zangu kwa Mafia Boxing Promotion kwa kuweza kunipa nafasi ya kuendeleza kipaji changu lakini imekuwa ikiangalia mabondia ambao wapo chini lakini wanamalengo na hasira na mchezo ndiyo wanapa nafasi kama ilivyo upande wangu,” anasema.