Bwenzi afunga tena, aiokoa KenGold jeshini

Bao la dakika ya 84 lililowekwa kimiani na kiungo mshambuliaji Seleman Rashid ‘Bwenzi’, limeinusuru KeGold kupoteza mchezo mwingine ikiwa ugenini baada ya kulazimisha sare ya 1-1 mbele ya JKT Tanzania kwenye Uwanja wa Meja Isamuhyo, uliopo jijini Dar es Salaam.

Hilo lilikuwa ni bao la tano kwa nyota huyo katika mechi sita tangu kurejea kwa duru la pili la Ligi Kuu Bara, akiwa pia na asisti moja katika mechi hizo, licha ya KenGold kuendelea kusalia mkiani japo imeongeza pointi nyingine moja kibindoni.

Katika mechi hiyo kali, JKT ndio iliyokuwa ya kwanza kupata bao sekunde chache kabla ya mapumziko baada ya Edward Songo kufunga kwa mkwaju wa penalti kutokana na kiungo Abdallah Masoud ‘Cabaye’ kutasfiriwa ameushika mpira wakati akiokoa kwa kichwa.

Licha ya wachezaji wa KenGold kumlalamikia mwamuzi wa mchezo huo juu ya tukio hilo, lakini penalti hiyo ilipigwa kwa Songo kumchambua kipa Mussa Mussa.

Kipindi cha pili timu zote zilifanya mabadiliko na kuongeza kasi ya mchezo huku wageni, KenGold wanaoshiriki Ligi Kuu kwa mara ya kwanza msimu huu wakionekana kuchangamka zaidi na haikuwa ajabu kupata bao la kusawazisha lililofungwa kwa shuti kali na Bwenzi baada ya gonga za hapa na pale na wachezaji wa timu hiyo.

Hiyo ilikuwa ni sare ya sita kwa KenGold iliyofikisha pointi 15 na ya tisa kwa maafande wa JKT inayomiliki pointi 27 kwa sasa ikiwa nafasi ya sita.

Ligi hiyo itaendelea tena saa 1:00 usiku wakati wenyeji Azam FC itakapoikaribisha Namungo kwenye Uwanja wa Azam Complex.