
NYOTA wa KenGold, Selemani Bwenzi amesema licha ya kikosi hicho kuendelea kusalia mkiani mwa Ligi Kuu Bara na pointi 15, lakini kuna matumaini makubwa ya kukinasua na janga la kushuka daraja kutokana na ushirikiano uliopo wa wachezaji.
Bwenzi aliyejiunga na kikosi hicho katika dirisha dogo la Januari mwaka huu akitokea Mbeya Kwanza, alisema mwenendo wao sio mbaya katika michezo ya hivi karibuni, jambo linalowapa matumaini ya kufanya vizuri kutokana na michezo kuwa mingi.
“Bado tuna nafasi nzuri sana ya kutoka chini tulipo na kusogea juu kwa sababu ukiangalia gepu la pointi na washindani wetu sio kubwa. Kikubwa ni kuendeleza huu ushirikiano tuliokuwa nao kwani kwa michezo iliyobaki inawezekana kabisa,” amesema.
Bao alilolifunga nyota huyo katika sare ya 1-1 dhidi ya JKT Tanzania Februari 27 limemfanya kuendeleza rekodi bora ya ufungaji kikosini, kwani hadi sasa ndiye anayeongoza baada ya kufunga matano na kutoa asisti moja.
Kabla ya kujiunga na KenGold, nyota huyu alikuwa Mbeya Kwanza inayoshiriki Ligi ya Championship aliyoifungia bao moja na kuchangia mengine mawili, ambapo hadi sasa amekuwa muhimili wa timu hiyo inayopigania kutoshuka daraja.
Kiwango bora cha Bwenzi kimemfanya kuwa miongoni mwa wachezaji waliosajiliwa dirisha dogo na kufanya vizuri kama ilivyo kwa mshambuliaji wa Singida Black Stars, raia wa Ghana, Jonathan Sowah aliyefunga mabao sita Ligi Kuu Bara.
Sowah aliyejiunga na Singida akitokea Al-Nasr Benghazi ya Libya amekuwa katika kiwango bora akiwa na kikosi hicho cha mjini Singida kwani mabao hayo ameyafunga katika michezo sita akiwa na wastani wa kufunga bao moja kwenye kila mchezo.