
Dar es Salaam. Taasisi ya Twaweza Afrika Mashariki imetangaza uteuzi wa Anna Bwana kuwa Mkurugenzi Mtendaji wake mpya, kuanzia Mei 15, 2025.
Bwana, mwenye uzoefu katika masuala ya utawala, anachukua nafasi ya Aidan Eyakuze, ambaye amekwenda kuiongoza Taasisi ya Open Government Partnership.
Uteuzi wa Bwana unatokana na mchakato wa kuteua viongozi uliofanyika kwa kina, ukilenga kupata kiongozi mwenye uwezo wa kuendeleza dhamira ya taasisi hiyo.
Akiwa na uzoefu wa zaidi ya miaka 15 katika kubuni na kutekeleza mipango ya kiutawala inayobadilika, anakwenda na utaalamu huo katika kubuni mikakati, maendeleo ya taasisi na uongozi wa timu.
Kwa sasa, akihudumu kama Mkurugenzi Mkazi wa BBC Media Action nchini Tanzania, Bwana ameshika nafasi muhimu za uongozi katika maeneo mbalimbali ya Afrika Mashariki, ikiwemo Ethiopia.
Majukumu yake ya awali ni pamoja na Naibu Kiongozi wa timu katika Mradi wa Taasisi za Maendeleo Jumuishi, Mshauri wa Masuala ya Utawala katika Ubalozi wa Ireland na Meneja wa Programu za Utawala katika Shirika la Oxfam Tanzania.
Kitaaluma, Bwana ana shahada ya kwanza ya Uchumi na Maendeleo kutoka Shule ya Uchumi ya London (LSE) na shahada ya pili katika Sera za Umma na Usimamizi kutoka Shule ya Masomo ya Asia na Afrika (SOAS).
Kazi yake imejikita zaidi katika utawala na uwajibikaji. Alianza kazi mwaka 2010 na Oxfam, ambapo alibuni, kutekeleza na kusimamia mradi wa uraia hai katika Kanda ya Ziwa na Ngorongoro.
Alifanya kazi pia na Ubalozi wa Ireland nchini Tanzania na Shirika la Irish Aid kama Meneja wa Programu za Utawala.
Vilevile, alihudumu kama Naibu Kiongozi wa timu wa SNV, mradi uliozingatia taasisi za maendeleo jumuishi na hivi karibuni, alikuwa Mkurugenzi Mkazi wa BBC Media Action nchini Tanzania tangu mwaka 2020, akishughulikia pia Ethiopia kwa muda wa miezi sita.
“Nimepata fursa ya kufanya kazi katika nchi mbalimbali, jambo lililonisaidia kutambua umuhimu wa muktadha, maarifa ya ndani, na haja ya kushughulikia changamoto kwa kutumia mifumo na mbinu za nchi husika.
“Wakati huo, kazi yangu imenisaidia kujifunza kutoka nchi mbalimbali, na ninaamini hili litaendelea kusaidia namna Twaweza inavyofanya kazi,” alisema Bwana.
Alisisitiza kuwa uzoefu wake unajumuisha ngazi za chini kabisa, akifanya kazi na mashirika ya kijamii, vikundi vya wakulima na wafanyakazi shuleni, hadi ngazi za kitaifa na kikanda, akishawishi taasisi za serikali na mifumo.
Mwenyekiti wa Bodi ya Twaweza, Bahame Nyanduga alionyesha imani katika uongozi wa Bwana, akisema: “Anna ni kiongozi huru tunayemhitaji kwa sasa. Ana ujuzi mkubwa katika uchambuzi wa uchumi wa kisiasa, utawala wa serikali na raia, na ubunifu katika kubuni na kusimamia programu.
“Uzoefu wake mpana katika mambo ya uraia, kitaifa na kimataifa, unamuweka katika nafasi nzuri ya kuongoza juhudi za Twaweza katika kanda hii, hasa tunapofanya kazi kwa karibu na Serikali.”
Mkurugenzi Mtendaji anayemaliza muda wake, Aidan Eyakuze, alisema, “Nashukuru kwa uteuzi wa Anna. Nilifanya naye kazi hapo awali, na naweza kuthibitisha uadilifu wake, fikra za kimkakati, ubunifu, na uwezo wa kutekeleza mambo. Sina shaka kwamba ataipeleka Twaweza kwenye ngazi mpya.”