Burna Boy na J Cole ni damu damu

Dar es Salaam. Mkongwe wa muziki wa Hip-Hop nchini Marekani J Cole amemualika staa wa Afrobeat kutokea Nigeria ‘Burna Boy’ nyumbani kwake North Carolina ambapo kuna studio yake ya nyumbani na imeripotiwa wawili hao wanarekodi nyimbo mbili.

Inaelezwa kuwa wawili hao bado wapo studio wanaendelea kuzifanyia kazi nyimbo hizo mbili. Ambapo moja itawekwa kwenye albamu mpya ya Burna Boy inayotarajia kutoka hivi karibuni itakayofahamika kama ‘No Sign Of Weakness’. Na ngoma ya pili itawekwa kwenye project mpya ya J Cole.

J Cole anaukubali uwezo wa  Burna Boy, kwani amewahi kusema msanii huyo ni mmoja kati ya waimbaji wenye vipaji vikubwa hajawahi kuona mpaka kufikia hatua ya kumuita 2pac aliyezaliwa Afrika. 

Kuipata collabo na J Cole sio suala dogo kutokana na nafasi yake kwenye muziki. Lakini pia gharama za verse yake. Cole amewahi kusema msanii anatakiwa kujipanga na dola 2000 sawa na Sh 5,188,000 kwa kila neno atakaloweka kwenye verse ya msanii.

Hii inakuwa sio mara ya kwanza kwa wawili hao kushirikiana kwenye ngoma ya pamoja utakumbuka mwaka 2023, Burna Boy alimshirikisha J Cole kwenye wimbo wake wa Thanks unaopatikana kwenye Albamu yake ya I Told Them iliyotoka Agosti 28, 2023.