Kenya. Mwanamuziki wa Nigeria, Burna Boy Machi 1, 2025 alifanya onyesho la muziki ambalo limeacha historia katika mji wa Nairobi nchini Kenya.
Tamasha hilo lilitawaliwa na amani likionesha umahiri wa Burna kutoa burudani ambayo mashabiki wengi wameisifia kuwa miongoni mwa utumbuizaji bora kuwahi kutokea nchini humo.

Kivutio kikubwa katika onyesho hilo ni baada ya wasanii waliokuwa wakiunda kundi la Sauti Sol Kenya, kuingia kwa kushtukiza na kuungana na Burna Boy jukwaani na kutumbuiza wimbo wa ‘Time Flies’ waliyoshirikishwa na msanii huyo kutoka kwenye albamu yake ya Twice As Tall iliyotoka Agosti, 13, 2020.
Hii inakuwa mara ya kwanza kwa Burna Boy kutumbuiza Live wimbo huo na Sauti sol tangu kuachiwa kwake miaka mitano iliyopita na kupelekea mashabiki kusifu kuwa ni wakati wa kihistoria kwa muziki wa Kenya.
Tiketi za viingilio kwa VVIP katika tamasha hilo ziliuzwa kwa Ksh 65,000 na ukumbi ulijaa. Lakini pia inaripotiwa kuwa Burna Boy amelipwa dola milioni 1 zaidi ya Sh 3 bilioni, huku akisafiri na timu ya watu 61 ambao ni pamoja na madansa, watu wa mitindo, ulinzi na watu wa bendi, yote hiyo ni kuhakikisha tamasha hilo linakuwa la kuvutia.

Kwa ufupi, tamasha la Burna Boy lililofanyika Uhuru Garden katika mji wa Nairobi, Kenya lilikuwa la aina yake na la kukumbukwa.
Hata hivyo, Msanii Harmonize alikuwa mmoja wa walio hudhuria shoo hiyo na alitakiwa kutumbuiza pamoja na Burna Boy lakini kutokana na kutofika kwenye maandalizi ya pafomance hiyo hakuruhusiwa kupanda jukwaani.

Utakumbuka Mei 2023, kundi la Sauti Sol lililokuwa likiundwa na mastaa wa kiume wa nne kutoka Kenya, Bien-Aime, Willis Chimano, Polycarp Otieno na Savara Mudigi, lilitangaza kutengana baada ya kuwa pamoja kwa miaka 20. Utengano huo ulikuja baada ya kumaliza ziara yao Desemba 16, 2023.