
Mstaafu wetu ana wazo. Inawezekana wazo lake hili linatokana zaidi na maumivu yake ya kuishia kuisikia kwenye bomba tu nyongeza yake ya Shilingi elfu hamsini ya pensheni yake iliyotangazwa kwa bashasha na Serikali toka Oktoba mwaka jana, na mpaka Mei mwaka huu imeishia kuwa hadithi ya Alfu lela ulela, na miayo tu.
Maumivu haya yanatokana zaidi na Serikali iliyotoa ahadi hiyo ya nyongeza ya pensheni kwa wastaafu, haijajitokeza kwa bashasha kutoa maelezo ya kile ilichokuwa wameahidi kwa wastaafu kimeishia kwa wastaafu kupata Sh 7,000 hadi Sh 10,000 badala ya Sh 50,000 iliyoahidi na Serikali mwaka jana, na badala yake ghafla kila Mheshimiwa amekuwa bubu, labda kwa sababu linahusu wastaafu!
Wastaafu tumeishia kupapasa huku na kule ili kujua ni wapi nyongeza yetu iliyotangazwa kwa bashasha na Serikali imeishia! Kama ni kikokotoo, Serikali ituambie kwa nini imetupa wastaafu Shilingi elfu hamsini kwa mkono wa kulia, halafu kwa mkono wa kushoto ikatumia kikokotoo kuchukua Shilingi elfu arobaini na kutuachia wastaafu Shilingi elfu kumi!
Hivi unaitozaje kikokotoo pensheni ya mstaafu?
Mstaafu wetu anatapatwa na wasiwasi kwamba hii labda inatokana na kwamba wenye hii nchi, ambayo waheshimiwa sasa wanaruhusiwa kula urefu wa kamba zao mradi hawapigi kelele.
Shilingi elfu arobaini zetu zimechepushwa kwenda kwenye urefu wa kamba ya mjanja mmoja anayejiandaa kwa uchaguzi mkuu, huku akisahau kuwa hata wastaafu kura zao zinahesabika, pamoja na kwamba zinatoka kwa wazee!
Mstaafu wetu ana wazo, japo ana wasiwasi kuwa litakataliwa na waheshimiwa wengi ambao ni watumishi wa Serikali inayopenda kujinasibu kwamba inaboresha maisha ya mstaafu, ili aweze kukabiliana na hali ngumu ya maisha, licha pia ya kwamba halimuumizi mheshimiwa yoyote, maana hela hazitoki mfukoni mwake!
Wazo liko hivi. Muda mchache ujao, Bunge la Taifa litavunjwa rasmi ili wananchi wajiandae kwa uchaguzi mkuu. Huu ni ule wakati wa kucheza ‘ngoma’ za kienyeji au kunywa ‘matapu tapu’ ya kienyeji na wananchi wao. Wabunge watapokea ‘kiinua mgongo’ chao cha mamilioni kadhaa kwa ajira ya miaka mitano waliyofanya!
Mstaafu anaishia kuona wivu maana yeye, baada ya miaka 40 ya ajira ya kujenga Taifa lake kweli bila maneno meengi, aliishia kupata ‘kishusha mgongo’ cha vimilioni visivyofika hata namba ya miaka aliyoajiriwa 40.
Sasa anaishia kujiuliza kwa nini hakuwa mbunge wakati sifa ya kuwa mbunge ni kujua kusoma na kuandika tu… Sasa hivi labda na kujua kuongea vyema na wananchi, hasa wakati huu wa uchaguzi!
Haya, Bunge litavunjwa ili kupisha uchaguzi mkuu. Hii ina maana kuwa kwa miezi mitatu, Bunge litakuwa halina wabunge.
Nchi ina wabunge wapatao 350 na zaidi kidogo, wanaopokea Shilingi zinazofika milioni 16 kwa mwezi, ukijumlisha marupurupu na marapurapu mengine ya wabunge hao.
Hii ina maana nchi inatoa Shilingi milioni 16 mara 350 kwa mwezi kulipa mishahara ya wawakilishi hao wanaosemekana kuwa ni wa wananchi.
Mstaafu anawaomba mumruhusu asitaje jumla ya hela hizo, asije akapata shinikizo la damu bure, wakati hana matibabu ya bure!
Kwa miezi mitatu ambayo wabunge watarajiwa watakuwa hawapo bungeni bali wako majimboni wakicheza ‘ngoma’ za kienyeji na sisi, wakitafuta kura ili warudi tena bungeni kwenye mshahara wa Shilingi milioni 16 kwa mwezi, pesa hizo zinategemewa kuwa zinawasubiri au zikifanya mambo mengine muhimu ya taifa. Rudia hapo, mambo mengine muhimu ya Taifa!
Wastaafu tunamuomba mheshimiwa Rais kuwa moja ya mambo muhimu ya Taifa hayo yanapaswa kuwa ni kuchukua japo robo tu, rudia hapo mheshimiwa Rais japo robo tu ya mishahara ya wabunge, na kuwapa wastaafu wetu walioteseka vya kutosha, na ambao keki ya Taifa waliyoipika wanaishia kuisikia harufu tu!
Mheshimiwa Rais, robo tu ya mishahara ya wabunge kwa miezi mitatu wasiyokuwepo unaweza kuwapa wastaafu kwa kigezo chochote kile unachoona kitafaa, iwe ni nyongeza ya pensheni ya Shilingi laki tano kwa mwezi, au iwe ni kuwapa wastaafu Shilingi milioni kumi moja kwa moja wakiwa hai, badala ya kungoja wafariki ndipo wategemezi wao wapewe Shilingi milioni tano — kama watapewa! Maana Shilingi elfu hamsini tu za nyongeza ya wastaafu zimewatoa watu imani, sembuse milioni tano je?
Hizi tunategemea kwamba zitafika mikononi kwa wastaafu wenyewe, maana zimetoka moja kwa moja mikononi mwa mheshimiwa Rais mwenyewe, tofauti na zile elfu hamsini ambazo zimeishia kuwa hadithi ya Alfu lela ulela!
Mheshimiwa Rais, nchi sasa iwafanyie wastaafu kile mtoto anachopaswa kuwafanyia wazazi wake, kuwajali na kuwashukuru kwa kumkuza na kumlinda hadi kuwa mtu mzima anayejitambua, ili waende Kinondoni kwa amani. Nchi ifanye hivyo kwa wastaafu wake.