
Dar es Salaam. Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo imetoa agizo kwa serikali kuhakikisha ukarabati wa uwanja wa Benjamin Mkapa unakamilika ifikapo Aprili 2025, ili uweze kukidhi viwango vya kimataifa kwa ajili ya mashindano ya Chan 2024 na Afcon 2027.
Azimio hili limetolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Husna Sekiboko, alipokuwa akiwasilisha taarifa ya shughuli za kamati hiyo kwa mwaka wa fedha 2024 hadi 2025, katika kikao cha Bunge kilichofanyika leo Februari 11, 2025 jijini Dodoma.
Katika hatua nyingine, Sekiboko ameipongeza serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuongezea bajeti wizara za Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Habari, Utamaduni na Michezo, jambo lililosaidia kufanikisha utekelezaji wa miradi mingi kwa ufanisi.
Hata hivyo Sekiboko, ameiomba serikali kuhakikisha inatekeleza miradi inayoendelea kwa wakati ili kuleta maendeleo ya haraka kwa Taifa na Jamii kwa ujumla.
Fainali za Chan 2024 zilikuwa zifanyike kuanzia Februari Mosi hadi Februari 28 mwaka huu lakini kamati ya utendaji ya Caf iliamua kuzisogeza mbele hadi Agosti mwaka huu.
Taarifa ambayo ilitolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) ilisema kuwa fainali hizo zilisogezwa mbele kutokana na kutokamilika kwa maandalizi yake.
Hata hivyo Tanzania kupitia kwa mwenyekiti wa kamati ya ndani ya maandalizi ya mashindano hayo, Leodgar Tenga alisema kuwa Uwanja wa Benjamin Mkapa umekamilika kama ilivyo kwa Uwanja wa New Amaan Zanzibar.
“”Ili kufanikisha mashindano hayo, Serikali imefanya maandalizi muhimu ikiwemo ukarabati na ujenzi wa miundombinu kwa ajili ya mashindano hayo ambao
umefanyika katika Uwanja wa
Benjamini Mkapa na Uwanja wa New Amaan Stadium Zanzibar.
“Vilevile kwa matakwa ya CAF vimejengwa viwanja vya mazoezi vya Gymkhana, Law School na Meja Jenerali Isamuhyo ambavyo vitatumika kwenye mashindano ya CHAN.
“Maandalizi haya ya miundombinu hii ya yamefikia asilimia zaidi ya tisini na tano,” alisema Tenga.