
Baraza la Taifa, ambalo ni sawa na Bunge la Seneti nchini Algeria, limetangaza siku ya Jumatano Februari 26 “kusitishwa kwa uhusiano wake” na Bunge la Seneti la Ufaransa, ili kupinga ziara ya rais wa Bunge la Seneti la Ufaransa Gérard Larcher katika Sahara Magharibi siku ya Jumatatu na Jumanne, eneo ambalo Algeria inaunga mkono waasi wa Polisario dhidi ya Morocco.
Imechapishwa:
Dakika 1
Matangazo ya kibiashara
Akiwasili siku ya Jumatatu, Februari 24 huko Laayoune, jiji kuu la Sahara Magharibi, Gérard Larcher, kiongozi mkuu nambari mbili katika taifa la Ufaransa, alibinisha uhusiano wa Ufaransa na Morocco, wakati Rachida Dati, Waziri wa Utamaduni, alizungumza juu ya ziara ya “kihistoria” katikati mwa mwezi wa Februari alipozuru Sahara Magharibi kwa mara ya kwanza.
Ziara hizo zinafuatia mabadiliko makubwa ya Rais Emmanuel Macron mnamo mwezi wa Julai 2024, na kuvunja msimamo wa jadi wa Ufaransa wa kushikamana na Umoja wa Mataifa. Paris imetoa uungaji mkono mkubwa kwa mpango wa kujitawala kwa eneo hili “chini ya uhuru wa Morocco” uliopendekezwa na Rabat, na kuchochea hasira ya Algiers.
Koloni la zamani la Uhispania la Sahara Magharibi, eneo kubwa la jangwa linalochukuliwa kuwa eneo lisilo na hadhi isiyojulikana na Umoja wa Mataifa, linadhibitiwa karibu 80% na Morocco, lakini limekuwa likidaiwa kwa miaka 50 na waasi wa Polisario Front, wakiungwa mkono na Algeria.
“Uungaji mkono wa Ufaransa kwa mpango wa kujitawala chini ya mamlaka ya Morocco kama mfumo pekee wa suluhu sasa umetolewa,” alisema Bw. Larcher, kabla ya kuongeza: “Sasa ni sera ya Jamhuri ya Ufaransa.”
Ikishutumu “ziara isiyo ya kuwajibika, ya uchochezi na ya kujionyesha, ofisi ya Baraza la Taifa (Bunge la Seneti la Algeria), chini ya rais Salah Goudjil, inatangaza kusitishwa mara moja kwa uhusiano wake na Bunge la Seneti la Jamhuri ya Ufaransa, ikiwa ni pamoja na itifaki ya ushirikiano wa bunge iliyotiwa saini Septemba 8, 2015,” Baraza la Taifa la Algeria limetangaza katika taarifa kwa vyombo vya habari.