Bulaya aipongeza Chadema, awataja Lissu na Mbowe bungeni

Dodoma. Mbunge wa Viti Maalumu, Esther Bulaya amekipongeza Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa kuendesha uchaguzi wa ndani kwa uwazi na kufuata misingi ya demokrasia.

Bulaya ametoa pongezi hizo leo Alhamisi Februari 13, bungeni jijini Dodoma wakati wa mjadala wa taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) kwa kipindi cha Februari 2024 hadi Januari 2025.

Chadema ilifanya mkutano mkuu wa uchaguzi Januari 21 na kumalizika Januari 22, 2025 katika ukumbi wa mikutano ya Mlimani City jijini Dar es Salaam.

Katika uchaguzi huo, Freeman Mbowe aliyekiongoza chama hicho kwa miaka 21 alishindwa na Makamu wake-bara, Tundu Lissu aliyepata kura 513 sawa na asilimia 51.5 huku Mbowe akipata kura 482 sawa na asilimia 48.3. Charles Odero yeye aliambulia kura moja kati ya kura 999 zilizopigwa na kura tatu kuharibika.

Kabla ya matokeo kutangazwa ukumbini, Mbowe alitumia ukurasa wake wa kijamii wa X kuandika: “Nimepokea kwa mikono miwili maamuzi ya uchaguzi wa Mkutano Mkuu wa chama chetu Chadema uliohitimishwa leo asubuhi 22 Januari 2025. Nampongeza Tundu Lissu na wenzake kwa kuaminiwa kutwikwa jukumu la uongozi wa chama. Nawatakia kila la kheri katika kukipeleka mbele chama chetu.”

Baada ya kutangazwa kwa matokeo, Mbowe alizungumza na wajumbe wa mkutano mkuu akiwapongeza kwa uamuzi uliofanyika na kuwataka kuungana katika kukijenga chama na kuwapa ushirikiano viongozi wapya.

Leo Alhamisi, Februari 13, 2025, Bulaya ametumia sehemu ya mchango wake bungeni kuzungumzia uchaguzi huo akimpongeza Lissu kwa kuchaguliwa kuongoza chama hicho na kusisitiza ana uwezo mkubwa wa kukifikisha katika demokrasia ya kweli.

“Kwa moyo wa dhati, napongeza Chadema kwa kuonyesha mfano wa uchaguzi huru na haki. Pia nampongeza Mheshimiwa Freeman Mbowe kwa kukubali matokeo na kuweka mbele maslahi ya demokrasia,” amesema Bulaya.

Ameongeza Lissu ana uzoefu mkubwa wa uongozi ndani ya Chadema, akihudumu kama makamu mwenyekiti, mnadhimu wa kambi rasmi ya upinzani bungeni, na mwanasheria mkuu wa chama.

“Historia yake inaonyesha ana sifa na uwezo wa kuongoza chama na kutufikisha kwenye demokrasia ya kweli,” amesisitiza Bulaya.