Brighton yaichapa Liverpool, yakaribia Conference League

Brighton yaichapa Liverpool, yakaribia Conference League

Brighton, England. Mabingwa wa Ligi Kuu ya England, Liverpool, wamejikuta wakikumbwa na kichapo cha mabao 3-2 kutoka kwa Brighton katika mchezo wa Ligi Kuu England uliochezwa jana Jumatatu, Mei 19 kwenye Dimba la American Express.

Liverpool walitangulia mapema dakika ya tisa kupitia kinda Harvey Elliott, aliyeunganisha pasi  ya Conor Bradley. Hata hivyo, Brighton walisawazisha dakika ya 32 kupitia kwa Yasin Ayari.

Katika muda wa nyongeza kipindi cha kwanza, kiungo mshambuliaji Dominik Szoboszlai alirejesha uongozi kwa Liverpool kwa bao la pili, akihakikisha wanaenda mapumziko wakiwa mbele.

Lakini kipindi cha pili kiligeuka kuwa cha Brighton baada ya Mjapani Kaoru Mitoma, aliyeingia kama mchezaji wa akiba, akisawazisha katika dakika ya 69.

Dakika ya 85, kijana wa miaka 17, Jack Hinshelwood, aliyetokea benchi katika dakika ya 84, alipachika bao la ushindi ingawa awali bao lake lilitupiliwa mbali kwa madai ya kuotea lakini VAR ikathibitisha bao hilo lilikuwa halali.

Kwa ushindi huo wa mabao 3-2, Brighton imesogea mpaka nafasi ya nane kwenye msimamo wa ligi, na sasa inahitaji alama moja tu dhidi ya Tottenham Hotspur ili kufuzu kucheza Europa Conference League msimu ujao.

Liverpool hadi sasa imeruhusu vipigo vinne msimu huu, baada kupoteza dhidi ya Nottingham Forest, Fulham, Chelsea na Brighton huku ikibakiza mchezo mmoja utakaofanyika kwenye Uwanja wa Anfield Jumapili, Mei 25 mwaka huu itakapokuwa na kibarua kingine dhidi ya Crystal Palace.

Katika mchezo huo, Majogoo wa Anfield watakabidhiwa taji la ubingwa wa EPL msimu huu kwa mara ya kwanza mbele ya mashabiki wao tangu mwaka 1992, ambapo mwaka 2020 walipewa taji hilo bila kuwepo kwa mashabiki kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa Covid-19.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *