BoT yaonya tena biashara ya upatu

Dar es Salaam. Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba ametoa onyo kwa wanaojihusisha, kuendelea kufanya biashara ya upatu akisema shughuli hizo ni haramu kwani zinafanyika pasipokuwa na uwiano wa shughuli za kiuchumi.

Tutuba anayasema hayo wakati baadhi ya watu wakitiwa nguvuni na Jeshi la Polisi kutokana na kujihusisha na biashara hiyo bila ya kuwa na kibali cha BoT wakiwemo wafanyakazi wa Kampuni ya Leo Burnett London (LBL).

Jumla ya wafanyakazi 38 wa LBL katika mikoa ya Dar es Salaam, Mbeya na Morogoro wametiwa nguvuni na BoT kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi.

Ambapo kampuni hiyo inadaiwa kuwachangisha wanachama wake Sh50,000 ada ya kiingilio ili wapate faida ya kila siku kwa kusambaza vipande vya video wanazotumiwa.

Gavana Tutuba, amesema mtu anayefanya upatu kwa kukusanya fedha ili awagawie wachache kwa kiwango kikubwa, kwa lengo la kuwavutia walete fedha zao pasi na kuwa na biashara ya kiuchumi ni kosa kisheria na taratibu za nchi.

Hii si mara ya kwanza kwa Gavana Tutuba kutoa onyo kwa wanaojihusisha na biashara za upatu. Amekwisha kuonya mara kadhaa na kutangaza hatua kali kwa kuchukuliwa kwa wote watakaojihusisha pasipo kuwa na sheria 

Leo Jumanne, Machi 4, 2025, Tutuba ametoa tena onyo alipozungumza na waandishi wa habari baada ya kuhutubia mkutano wa Umoja wa Mabenki Tanzania (TBA), uliofanyikia jijini Dar es Salaam.

 “Niendelee kuwaonya watu wanaofanya shughuli hii kwa kuwaibia wananchi pasipokuwa na uelewa kwamba waache mara moja. Mtu yeyote anayekusanya fedha kwa upatu ni haramu. Tunaendelea kuwakamata kwa kosa la kuwaibia wananchi kuwalaghai na kupoteza fedha zao, kufanya hivyo sio utaratibu rasmi’ ameonya vikali.

Akifafanua zaidi amesema shughuli yeyote ya kiuchumi halali inapaswa iendane na utekelezaji wa majukumu yanayochangia kwenye za uchumi.

Amesema wananchi wapaswa kutumia huduma rasmi kwa taasisi zilizopewa dhamana na leseni ya BoT zikiwemo Benki, taasisi ndogo za kifedha, mitandao iliyosajiliwa na benki kuu pekee.

“Tumetoa fursa kwa vyama vya ushirika kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika watoe leseni ya kuendesha Saccos kwa niaba ya BoT, tumetoa pia kwa halmashauri kwa niaba ya BoT watoe leseni ya kuendesha taasisi ndogo za kijamii za wanachama (Vicoba).

“Hivyo mtu yeyote anayetaka kujishughulisha na huduma rasmi za kifedha lazima apate leseni kutoka BoT, Tume ya Maendeleo ya Ushirika au Halmashauri. Tofauti na hapo kama anasema amesajili tu anakuwa anahadaa kwani lazima apate leseni,” amefafanua.

Hali ya ukuaji wa uchumi nchini

Akizungumzia hali ya kiuchumi nchini, Gavana huyo amesema uchumi umeendelea kukua na hadi mwaka 2024 umefikia asilimia 5.4 ukilinganisha na ukuaji wa kidunia ambao ulikuwa ni asilimia 3.2, hivyo Tanzania imefanya vizuri.

“Mfumuko wa bei pia wastani wa mwaka jana tumekuwa na asilimia 3.1 ukilinganisha na mfumuko wa bei wa kidunia ambao ulikuwa asilimia 4.7,” amesema.

Katika utendaji na utekelezaji wa majukumu ya kiserikali, amesema suala la uwiano wa deni la na pato la Taifa kwa mwaka jana Desemba ilikuwa asilimia 41.1 ukilinganisha na ukomo unaokubalika wa asilimia 55 ambayo kwa uwiano huo Tanzania imefanya vizuri,” amesema.

Pia, hadi mwaka jana kiwango cha kutoa mikopo kwenye sekta binafsi imefikia asilimia 16.8 ukilinganisha na lengo la asilimia 15. ”Kiwango cha mikopo chechefu imefikia asilimia 3.3 ikiwa ni chini ya lengo la asilimia tano hivyo imepungua.

Kuhusu Umoja wa Mabenki

Gavana akielezea kuhusu mkutano huo wa tatu wa Jumuiya ya Mabenki Tanzania unaoangazia huduma jumuishi za kifedha kwa upande wa wananchi inawawia rahisi kufanya shughuli zao za kimaendeleo.

“Katika majadiliano kwenye mkutano huu wataangazia ujumuishaji wa kifedha na namna ya kufikisha huduma hizo kwa wananchi. Tunapoongelea kupata huduma rasmi za kifedha kwa sasa kuna asilimia 76 ndio wanaipata,” amesema.

Amesema ujumuishi wa huduma rasmi za kifedha Serikali imetengeneza mkakati wa uchumi wa kidijitali wa miaka 10 unaoanza 2024 hadi 2034, lengo ikiwa ni kutumia mifumo ya kidijitali kuweka mifumo mizuri ili kila Mtanzania apate huduma akuze kipato aondoe umasikini achangie na uchumi wa nchi.