Bosi WHO amlilia Dk Ndugulile

Dar es Salaam. Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa (WHO), Dk Tedros Adhanom Ghebreyesus ameeleza kushtushwa kwake na kifo cha Mkurugenzi mteule wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Kanda ya Afrika, Dk Faustine Ndugulile.

Dk Ndugulile aliyekuwa pia Mbunge wa Kigamboni, amefariki dunia usiku wa kuamkia leo Jumatano, Novemba 27, 2024 nchini India alipokuwa akipatiwa matibabu.

Ndugulile alichaguliwa kuwa Mkurugenzi kikanda wa Afrika katika Shirika la Afya Duniani (WHO), katika kikao cha 74 cha Kamati ya Kanda ya Afrika ya shirika hilo kilichofanyika nchini Congo Brazzaville Agosti 26 hadi Agosti 30, 2024 na alitarajiwa kumrithi Dk Matshidiso Moeti wa Botswana aliyemaliza muda wake.

Kupitia ukurasa wake wa X leo Novemba 27, 2024, Dk Ghebreyesus, ameandika,  “nimeshtushwa na kusikitishwa sana kwa taarifa za msiba wa ghafla wa Dk Faustine Ndugulile, Mkurugenzi Mteule wa Shirika la Afya Duniani. Salamu zangu za rambirambi kwa familia, Bunge na wananchi wa Tanzania.”

Dk Ghebreyesus ametoa salamu hizo akijibu salamu zilizotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan katika mtandao huo akitoa pole kwa Bunge la Jamhuri ya Muungano, familia, wananchi wa Kigamboni, ndugu, jamaa na marafiki.

Endelea kufuatilia Mwananchi.