Tel Aviv. Baraza la Mawaziri la Israel limeidhinisha kufukuzwa kazi kwa Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa (Shin Bet) huku maandamano yakiibuka upya kupinga uamuzi huo wa serikali.
Ronen Bar ambaye ameiongoza Shin Bet tangu 2021, atatakiwa kukabidhi ofisi Aprili 10, 2025 ama kabla ikitegemea wakati gani mrithi wake atakapokuwa ameteuliwa.
Al Jazeera imeripoti leo Ijumaa Machi 21, 2025 kuwa taarifa ya kuidhinishwa kufutwa kazi kwa Bar imethibitishwa na Ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu.

Netanyahu alitoa pendekezo la kufutwa kazi kwa Bar kwa kile alichodai kukosa imani naye kuhusiana na kinachoendelea kwenye mzozo wa Israel na wapiganaji wa kundi la Hamas eneo la Ukanda wa Gaza nchini Palestina.
Bar, ambaye ameongoza idara hiyo ya usalama wa taifa tangu mwaka 2021, alikataa kuhudhuria mkutano wa baraza la mawaziri uliokuwa ukijadili nafasi yake.
Katika barua iliyosambazwa na Shin Bet, Bar aliishutumu Serikali kwa kuendeshwa na mambo yasiyofaa na migongano ya maslahi ya kibinafsi na ya kitaasisi ya kiwango cha juu hususan kuhusiana na mzozo wa Gaza.
Hatua hii inakuja baada ya Netanyahu kusema Jumapili kuwa angewasilisha suala la kufutwa kazi kwa Bar kwenye baraza la mawaziri kutokana na kukosa imani na ofisa huyo wa usalama.
Netanyahu na Bar wamekuwa wakivutana kwa miezi kadhaa kutokana na mvutano kuhusu uchunguzi wa rushwa unaolenga Ofisi ya Waziri Mkuu na lawama kuhusu kushindwa kuzuia mashambulizi ya Hamas Oktoba 7, 2023.
Katika barua yake, Bar alisema kufutwa kwake kazi kulichochewa na tamaa ya kusitisha harakati za kutafuta ukweli kuhusu matukio yaliyotangulia kabla ya kuanza operesheni ya kijeshi ya Oktoba 7, 2023, eneo la Gaza.
Shin Bet, mapema mwezi huu, ilitoa ripoti iliyokiri kuwa ilipaswa kuizuia Hamas, huku ikimlaumu Netanyahu kwa kusaidia kuunda mazingira yaliyosababisha mashambulizi hayo ili kuanzisha vita dhidi ya kundi hilo la Hamas.
Pendekezo la Netanyahu la kumfuta kazi mkuu wa usalama lilikosolewa vikali na vyama vya upinzani na lilizua upya maandamano kutoka kwa raia wa Israel wanaoipinga Serikali yake ya mrengo wa kulia.
Alhamisi, polisi walitumia maji ya kuwasha na kuwakamata watu 12 baada ya mapambano na waandamanaji katika jiji la Tel Aviv na Jerusalem nchini humo.
Kwa mujibu wa takwimu rasmi zilizotolewa na Serikali nchini Israel, shambulizi la kushtukiza la Hamas la Oktoba 7, 2023 lilisababisha mauaji ya waisraeli takriban 1,139 huku zaidi ya 250 wakichukuliwa mateka.

Hata hivyo, kumekuwa na usiri juu ya hali halisi ya vifo na majeruhi wanaosababishwa na mashambulizi ya Hamas maeneo mbalimbali ya Israel, taarifa zimekuwa zikifichwa.
Baada ya Hamas kutekeleza uvamizi huo nchini Israel, jioni yake Netanyahu alitangaza kuanza operesheni ya kijeshi katika ukanda wa Gaza ambapo kupitia operesheni hizo, Wapalestina zaidi ya 49,547 wamethibitishwa kuuawa huku 112,719 wakijeruhiwa.
Hata hivyo, Wizara ya Afya eneo la Gaza imedai kuwa takwimu ya Wapalestina waliouawa katika mashambulizi hayo ya Israel huenda ikawa zaidi ya 60,000 kwani bado kuna mabaki ya watu yaliyonasa kwenye vifusi.
Mbali na mauaji hayo ya raia, Israel imesababisha uharibifu wa miundombinu na majengo sambamba na kuwalazimu wakazi wa Gaza zaidi ya milioni 2 kuyakimbia makazi yao.
Kufuatia makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya pande mbili za mzozo huo, yaliyofikiwa Januari 19, 2025, inaaminika bado mateka 59 wa Israel wanaendelea kushikiliwa Gaza huku zaidi ya 30 wakiachiwa huru.
Katika makubaliano hayo, raia wa Palestina waliokuwa wanashikiliwa kwenye magereza ya Israel zaidi ya 1,500 walinufaika kwa kuachiwa huru, huku awamu ya pili ya makubaliano hayo ikigonga mwamba, jambo ambalo limesababisha Israel kurejesha upya mashambulizi yake eneo la Gaza.
Al Jazeera imeripoti kuwa tangu kurejesha mashambulizi hayo Jumanne Machi 18, 2025, zaidi ya Wapalestina 600 wameuawa huku zaidi ya 200 wakiwa ni watoto.
Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa Mashirika.