Bosi wa Jatu atoa ombi mahakamani, Serikali kumjibu Machi 11

Dar es Salaam. Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Jatu PLC, Peter Gasaya (33), ameiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imfutie kesi inayomkabili na kumuachia huru kutokana na upelelezi wa shauri hilo kutokamilika tangu mwaka 2022, aliposhtakiwa.

Gasaya anakabiliwa na mashitaka mawili ambayo ni kujipatia Sh5.1 bilioni kwa njia ya udanganyifu na kutakatisha kiasi hicho cha fedha.

Mahakamani hapo

Gasaya kupitia wakili wake, Nafikile Mwamboma ametoa ombi hilo leo Alhamisi Machi 6, 2025 mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Geoffrey Mhini, wakati kesi hiyo ilipoitajwa.

Mwamboma amefikia hatua hiyo, baada ya Wakili wa Serikali,  Eva Kassa kudai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado unaendelea, hivyo wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Kassa baada ya kutoa taarifa hiyo ndipo wakili Mwamboma alipopinga ombi la kuahirishwa kwa kesi hiyo.

“Mheshimiwa hakimu, napinga ombi la upande wa mashitaka la kutaka kuahirisha kwa kesi hii, kwa sababu mshtakiwa alishafutiwa na kukamatwa tena na kufunguliwa kesi nyingine yenye mashitaka kama ya mwanzo,” amedai Mwamboma.

“Mheshimiwa hakimu, baada ya marekebisho ya sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, kifungu cha 91(3) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, kinaleta takwa, kama mshtakiwa ameachiwa kwa kosa lilelile, hawezi kukamatwa kwa kosa lilelile na hoja zilezile,” amedai Mwamboma.

Amesema sheria hiyo iliweka takwa moja kwa upande wa mashitaka wawe na ushahidi wa kutosha ndipo mshtakiwa akamatwe tena.

“Kukamatwa kwake tena kwa mara ya pili, kunamaanisha upande wa mashitaka wana ushahidi wa kutosha na kesi inapaswa kusikilizwa, hivyo hii sababu ya upelelezi kutokukamilika inashangaza,” amedai wakili na kuongeza.

“Sisi tunaamini upelelezi ulishakamilika na wana ushahidi wa kutosha kuendesha kesi hii,” amedai.

Mwamboma aliendelea kudai kuwa, pia Muongozo wa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) wa Septemba 20, 2022 kuhusu ufunguaji wa mashitaka na ukamilishaji upelelezi kwa makosa ya jinai unaeleza kuwa mshtakiwa hatakamatwa kama upelelezi haujakamilika.

“Na kesi hii ilitakiwa ikamilike upelelezi wake ndani ya siku 90 na kama haujakamilika, Mwendesha Mashtaka wa Mkoa anatakiwa kuomba kibali kwa DPP ili kukamilisha upelelezi, lakini hawajafanya hivyo,” ameendelea kudai wakili Mwamboma.

Mwamboma ameendelea kudai mshtakiwa alikamatwa na kufikishwa mahakamani hapo mwaka 2022, hivyo upande wa utetezi hawaoni kama ni busara kwa Mahakama kulifumbia macho jambo hilo kwa kigezo cha kutokukamilisha upelelezi.

“Hivyo, Mheshimiwa hakimu tunaomba mahakama yako ikatae ombi la kuahirisha kesi hii na badala yake iondoe mashitaka yanayomkabili mteja wangu na kumuachia huru mshtakiwa,” amedai.

Mwamboma baada ya kutoa hoja hizo, wakili Kassa aliomba Mahakama iwape muda upande wa mashitaka wawasilishe hoja hizo kwa wakili anayeendesha kesi hiyo ambaye ni Roida Mwakamale ili aje kuzijibu.

Hakimu Mhini amekubaliana na ombi hilo la upande wa mashitaka na kuahirisha kesi hadi Machi 11, 2025 kwa ajili ya upande wa mashitaka kuja kujibu hoja zilizotolewa na upande wa utetezi.

Mshtakiwa amerudishwa rumande kutokana na shitaka la kutakatisha fedha linalomkabili halina dhamana.

Katika kesi ya msingi, mshtakiwa anadaiwa, kati ya Januari Mosi, 2020 na Desemba 31, 2021 katika jiji la Dar es Salaam, akiwa kama Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni hiyo, kwa njia ya udanganyifu alijipatia Sh 5,139,865,733 kutoka Saccos ya Jatu.

Mshtakiwa anadaiwa kujipatia fedha hizo kwa njia ya udanganyifu kutoka Saccos ya Jatu kwa kujipambanua kwamba fedha hiyo ataipanda kwenye kilimo cha mazao, jambo ambalo alijua kuwa sio kweli.

Shitaka la pili ni kutakatisha fedha tukio analodaiwa kulitenda kati ya Januari Mosi, 2020 na Desemba 31, 2021 katika jiji la Dar es salaam.

Siku hiyo ya tukio na eneo hilo, mshtakiwa akiwa Mtendaji Mkuu na mwanzilishi wa Jatu Saccos, alijihusisha na muamala wa Sh5,139,865,733 kutoka katika akaunti ya Jatu Saccos iliyopo benki ya MNB tawi la Temeke kwenda katika akaunti ya Jatu PLC iliyopo katika benki ya NMB tawi la Temeke, wakati akijua fedha hizo zinatokana na kosa tangulizi la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Kwa mara ya kwanza Gasaya alifikishwa mahakamani hapo, Desemba 29, 2022 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi yenye mashitaka mawili ambayo ni kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kutakatisha fedha.