
Dar es Salaam. Mshtakiwa Peter Gasaya(33) ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Jatu PLC, anayekabiliwa na kesi uhujumu uchumi, ameiomba mahakama kesi yake isikilizwe kwa njia ya video mpaka hapo upelelezi wa kesi hiyo utakapokamilika.
Gasaya anakabiliwa na mashtaka mawili ambayo ni kujipatia Sh5.1bilioni kwa njia ya udanganyifu na kutakatisha kiasi hicho cha fedha, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Hii ni mara ya pili kwa mshtakiwa huyo kutoa ombi hilo, kwani mara ya kwanza ilikuwa ni Februari 10, 2025 ambapo alimuomba hakimu anayesikiliza kesi yake, sisaini hati yake ya kumtoa gerezani na kumpeleka mahakamani mpaka hapo upelelezi wa kesi yake utakapokamilika.
Gasaya ametoa ombi hilo baada ya upande wa mashtaka kuieleza Mahakama hiyo upelelezi wa kesi haujakamilika.
“Mheshimiwa hakimu, naomba kukumbushia ombi langu ambalo nililiwasilisha kipindi cha nyuma kuwa naomba kesi yangu iwe inatajwa kwa njia ya video bila mimi kuletwa katika Mahakama yako, mpaka hapo upande wa mashtaka watakapokamilisha upelelezi wao,” amedai Gasaya.
Baada ya kuwasilisha ombi hilo, Hakimu Mkazi Mwandamizi, Geofrey Mhini amemwambia Mahakama imelichukua ombi lake na litazimgatiwa pale itakavyowezekana.
Mhini baada ya kueleza hayo, ameahirisha kesi hiyo hadi Aprili 10, 2025 kwa kutajwa na mshtakiwa amerudishwa rumande kutokana na shtaka la kutakatisha fedha linalomkabili halina dhamana.
Awali, wakili wa Serikali Roida Mwakamele alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika, hivyo wanaomba tarehe nyingine kwa ajili kutajwa.
Kwa mara ya kwanza Gasaya alifikishwa katika Mahakamani hapo, Desemba 29, 2022 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi yenye mashtaka mawili ambayo ni kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kutakatisha fedha.
Katika kesi ya msingi, mshtakiwa anadaiwa, kati ya Januari Mosi, 2020 na Desemba 31, 2021 katika Jiji la Dar es Salaam, akiwa kama mkurugenzi mkuu wa kampuni hiyo, kwa njia ya udanganyifu alijipatia Sh5.13 bilioni kutoka Saccos ya Jatu.
Mshtakiwa wanadaiwa kujipatia fedha hizo kwa njia ya udanganyifu kutoka Saccos ya Jatu kwa kujipambanua kwamba fedha hiyo ataipanda kwenye kilimo cha mazao, jambo ambalo alijua kuwa siyo kweli.
Shtaka la pili ni kutakatisha fedha tukio analodaiwa kulitenda kati ya Januari Mosi, 2020 na Desemba 31, 2021 katika jiji la Dar es Salaam.
Siku hiyo ya tukio na eneo hilo, mshtakiwa akiwa Mtendaji Mkuu na mwanzilishi wa Jatu Sacoss, alijihusisha na muamala wa Sh5.13 bilioni kutoka katika akaunti ya Jatu Saccos iliyopo Benki ya MNB tawi la Temeke kwenda katika akaunti ya Jatu PLC liyopo katika benki ya NMB tawi la Temeke, wakati akijua fedha hizo zinatokana na kosa tangulizi la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.