Bosi mpya Tanesco atoa mwelekeo wake

Dar es Salaam. Mkurugenzi Mtendaji mpya wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Lazaro Twange anabainisha kile anachokwenda kukifanya ndani ya shirika hilo.

Usiku wa Mei 6, 2025, Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu ilitoa taarifa kwa umma juu ya uteuzi wa Lazaro Twange uliofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Twange aliteuliwa ili kujaza nafasi iliyokuwa wazi kufuatia kifo cha aliyekuwa mkurugenzi mkuu wa shirika hilo, Gissima Nyamo-Hanga aliyefariki dunia usiku wa kuamkia Aprili 13, 2025 katika ajali ya gari iliyotokea Bunda, mkoani Mara.

Kabla ya uteuzi huo, Twange alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, mkoani Dar es Salaam. Aidha, amewahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Babati, mkoani  Manyara na Mkuu wa Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro.

Pia, kabla ya kuwa mkuu wa wilaya hizo, aliwahi kuhudumu kama naibu mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) anayesimamia operesheni kabla ya kuondolewa katika nafasi hiyo mwaka 2017.

Umeme wa uhakika ndio kubwa ambalo wananchi wanalihitaji ili shughuli zoa za kiuchumi ziweze kufanyika bila kikwazo.

Bila kujali hali iliyopo ikiwemo ya hewa, wananchi wanataka ziwepo taarifa sahihi endapo kutakuwa na kukatika kwa umeme ili wajue namna ya kujiandaa.

Hoja ya kukatikakatika kwa umeme ilikuwa ni moja ya mijadala iliyotawala bajeti ya Wizara ya Nishati 2025/26 iliyowasilishwa bungeni Aprili 28 na 29, 2025.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko akihitimisha hoja yake alisema amepokea maoni na ushauri wa wabunge juu ya suala hilo la umeme kukatikakatika na wanakwenda kulifanyia kazi.

Leo Alhamisi, Mei 8, 2025 ikiwa ni siku mbili zimepita tangu uteuzi huo ufanyike, Mwananchi limemtafuta Twange na kuzungumza naye ambapo anaanza kwa kusema: “Kwanza kabisa namshukuru Rais Samia kwa kuniamini na kuniteua kunipa hii kazi kubwa na muhimu kwa Taifa letu.”

Kuhusu changamoto ya kukatika katika kwa umeme, Twange amesema: “Pamoja na mimi kuwa mtumishi wa Tanesco kwa sasa, mimi ni Mtanzania na mwananchi ambaye pia ninatumia huduma za maji, umeme, barabara na nyinginezo, kwa hiyo nafahamu wananchi wanahitaji huduma hii ya umeme wakati wote.”

“Wenzangu ambao nimewakuta wamefanya kazi kubwa, tutashirikiana kuhakikisha tunatumia akili tulizonazo, ubunifu, kusikiliza sana kutoka kwa wananchi na maelekezo kutoka kwa wananchi wetu kuhakikisha tunapunguza malalamiko na hali ya wananchi kukosa umeme,” anasema.

Katika kusisitiza hilo, Twange anasema: “Kazi ni ngumu lakini kwa ushirikiano na wadau mbalimbali mkiwemo ninyi waandishi wa habari tunaweza.”

Anasema ndani ya shirika hilo kuna mifumo mbalimbali ya kubadilishana taarifa kutoka kwao kwenda kwa wananchi lakini yote kwa yote: “Tutahakikisha tunafanya kazi kubwa kuhakikisha umeme unapatikana.”

Twange anasema suala la uwepo wa umeme kama ambavyo Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko alivyozungumza bungeni wakati wa mjadala wa bajeti ya Wizara ya Nishati kuhakikisha umeme unapatikana, kwani ndicho wananchi wanakitaka.

“Kama waziri alivyojibu bungeni hakuna mtumishi wa Tanesco anayefurahi wananchi kukosa umeme,” anasema.

Twange anasema kuna sababu mbalimbali za umeme kukatika ikiwemo za ndani na nyingine ziko nje ya uwezo wao ikiwemo za kibinadamu kama wananchi kuharibu miundombinu na au hali ya hewa.

“Umeme unaweza kukatika si sababu ya Tanesco bali shughuli zingine za kibinadamu kikubwa ni kushirikiana kila mmoja kwa nafasi yake kuhakikisha umeme unapatikana,” anasema.

Akijibu swali Watanzania watarajie nini kutoka kwake, anasema: “Muda utazungumza wenyewe lakini napenda kwenda ‘site’ kwani huko ndiko kuna wananchi na kazi zetu ziko huko, huduma za mitambo na tutakwenda sana huko.”

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti, Sera na Uchumi (Repoa), Dk Donald Mmari alipozungumza na Mwananchi juu ya uteuzi huo alisema jukumu kubwa lililopo mbele ya Twange ni kuhakikisha umeme wa uhakika na nafuu unakuwepo nchini.

Hiyo ni kutokana shughuli nyingi nchini ikiwemo uzalishaji viwandani kuhitaji umeme wa uhakika, ili waweze kuzalisha bidhaa zinazoweza kushindana sokoni.

“Viwanda vinataka umeme, wazalishaji wa mazao hasa bidhaa zinazoharibika wanataka uhakika umeme ili waweze kutunza mazao yao, watoa huduma mbalimbali wanataka umeme,” alisema Mmari na kuongeza.

“Uchukuzi sasa hivi tuna treni ya umeme nao wanataka umeme wa uhakika, kila kitu kinahitaji umeme wa uhakika na gharama nafuu hivyo hili ni jukumu kubwa lililo mbele yake,” alisema Dk Mmari.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *