Bosi Amsons: Kenya, Tanzania si washindani wa kiuchumi

Dar es Salaam. Tanzania na Kenya huenda zikawa na tofauti katika maeneo kadhaa, ikiwa ni pamoja na siasa, biashara, michezo, na utalii, lakini pia ni marafiki wazuri, imeelezwa.

Hilo limewekwa bayana na Mkurugenzi Mtendaji wa Amsons, Edha Nahdi, katika mahojiano yake ya kwanza ya kina tangu kumaliza ununuzi wa kampuni ya Bamburi Cement ya Kenya.

Nahdi katika mahojiano hayo amesema licha ya migogoro ya kawaida inayoshuhudiwa, nchi hizi mbili ni washirika na zimekuwa zikikubali wawekezaji kutoka pande zote mbili kwa furaha kubwa.

“Wengine wanaona Kenya na Tanzania kama maadui wakali, lakini ni dhana potofu kusema kuwa Watanzania na Wakenya hawawezi kushirikiana,” Nahdi amesema katika mahojiano na The Africa Report katika makala iliyo chapishwa Machi 19, 2025. Jarida hilo kutoka nchini Ufaransa, linalochapishwa kila robo mwaka likijikita katika siasa na uchumi wa Afrika.

Likimnukuu Nahdi akisema hilo limeshuhudiwa baada ya biashara na benki kadhaa za Kenya kama KCB na Equity kufanya kazi kwa mafanikio nchini Tanzania kwa miaka 14 au 15, pia kampuni kadhaa za Tanzania zimeweza kuingia kwa mafanikio katika soko la Kenya.

“Vivyo hivyo, tulipoingia Kenya, tulipokea msaada mkubwa kutoka kwa Serikali, mapokezi mazuri, na ushirikiano bora,” amesema Nahdi katika makala ya The Africa Report.

Alikiri kuwa Kenya ina kiwango cha maendeleo kikubwa kuliko Tanzania kwa ukubwa wa uchumi, huku akikubali kuwa uchumi wa Tanzania pia unapanuka kwa kasi.

“Hiyo haimaanishi hatupo katika hatua tofauti za maendeleo, Kenya ina uchumi uliokomaa na wa kisasa huku Tanzania ikiwa inakua kwa kasi na ipo katika hatua ya ukuaji mkubwa. Sekta nyingine tayari zimekuwa na kutoa fursa za kipekee, lakini kuwa maadui? Hapana, nchi zetu mbili si maadui,” amesema Nahdi.

Tanzania na Kenya, ambazo ni nchi zenye uchumi mkubwa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), mara nyingi hukumbwa na migogoro ya kibiashara, ikiwemo vizuizi visivyokuwa vya kikodi, lakini imekuwa ikipunguzwa.

Mapema mwaka 2024, Mamlaka ya Kilimo na Chakula ya Kenya (AFA) ilianzisha kodi ya asilimia mbili kwa nafaka na kunde, jambo lililosababisha malalamiko kutoka kwa wafanyabiashara wa Tanzania na kupelekea kuzuiwa kwa malori zaidi ya 40 kwenye mpaka wa Namanga.

Amsons imedhamiria kuwa mzalishaji mkuu wa saruji Afrika Mashariki, baada ya kununua Bamburi Cement kwa Sh427 bilioni mwaka 2024, kuwekeza Sh459.7 bilioni kununua hisa za asilimia 65 za Mbeya Cement mwaka 2023, na uwekezaji unaoendelea wa Sh840.66 bilioni kwenye kiwanda cha Bamburi clinkerisation huko Mombasa.

Hata hivyo, kulingana na The Africa Report, biashara za Afrika Mashariki kama Amsons Group zinaposhindania umaarufu katika sekta ya saruji ya kanda hii kupitia ununuzi mkubwa, zinakutana na ushindani mkubwa kutoka kwa kampuni kubwa za China.

“Kulikuwa na ushindani mkubwa,” alisema Nahdi katika mahojiano na The Africa Report. “Kampuni kutoka Afrika Kaskazini, India, na China zilikuwa na hamu kubwa ya mali hii, hivyo zabuni zilikuwa za ushindani mkubwa kifedha,”

Aliiambia The Africa Report kwamba Amsons walichukua karibu miaka miwili kufanya uchambuzi wa soko kabla ya kufanya uamuzi wa kuitwaa Bamburi.

Mbali na uwekezaji wa Sh840.66 bilioni katika kiwanda cha Bamburi clinkerisation huko Mombasa ambapo msingi unatarajiwa kuwekwa Oktoba na uzalishaji unatarajiwa kuanza baada ya miezi 24, Amsons pia inatazama fursa za ujenzi wa viwanda vipya vya saruji nchini Tanzania na pia inatazama fursa nchini Uganda.

“Uganda ni ndugu kwa Kenya na Tanzania, sisi sote ni sehemu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Nchini Uganda kuna fursa za ujenzi wa viwanda vipya na pia fursa za ununuzi,” alisema Nahdi. “Kwa sasa, kila kitu kiko mezani,” aliiambia The Africa Report.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *