Borrell: Hati ya kukamatwa Netanyahu, Gallant si ya kisiasa, nchi zote za EU zina wajibu wa kuitekeleza

Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya, Josep Borrell amesema, hati za zilizotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC za kuamuru kukkamatwa waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel Benjamin Netanyahu na waziri wa zamani wa vita wa utawala huo Yoav Gallant si maamuzi ya “kisiasa” na ni lazima “yaheshimiwe” na nchi zote wanachama wa umoja huo.

Katika hatua ya kihistoria, mahakama ya ICC yenye makao yake The Hague imetangaza kuwa imetoa waranti wa kukamatwa Netanyahu na Gallant kutokana na uhalifu wa kivita wanaotuhumiwa kuufanya katika maeneo ya Palestina, ikiwemo Ghaza.

“Sio uamuzi wa kisiasa … na uamuzi wa mahakama unapaswa kuheshimiwa na kutekelezwa,” amesema Josep Borrell katika mkutano na waandishi wa habari aliofanya pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jordan Ayman Safadi mjini Amman.

Borrell amesisitiza kuwa uamuzi huo ni “wa lazima,” na kwamba pande zote ambazo ni wanachama wa ICC, “zinazojumuisha nchi zote wanachama wa Umoja wa Ulaya,” ni lazima zitekeleze uamuzi huo.

Josep Borrell

Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC imeeleza katika uamuzi wake kwamba “imepata sababu za kuridhisha” kuamini kwamba Netanyahu na Gallant wanabeba dhima ya jinai ya kuhusika na “uhalifu wa kivita wa kutumia njaa kama silaha ya kivita pamoja na uhalifu dhidi ya ubinadamu wa mauaji, mateso, na vitendo vingine vya kinyama” dhidi ya Wapalestina.

Waranti wa ICC umetolewa hapo jana wakati vita vya kinyama na mauaji ya kimbari yanayoendelea kuufanywa na utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Ghaza yameingia katika mwaka wake wa pili hivi majuzi yakiwa tayari yameshaua Wapalestina 44,000 wengi wao wakiwa wanawake na watoto.

Mashambulizi hayo ya Israel yamewafanya karibu wakazi wote wa Ghaza wakimbizi waliolazimika kuhama makazi yao huku kukiwapo na mzingiro wa makusudi unaoendelea kuwekwa na utawala huo dhalimu ambao umesababisha uhaba mkubwa wa chakula, maji safi na dawa, na kuwafanya Wapalestina wa eneo hilo wakabiliwe na baa kubwa la njaa…/