
Josep Borrell Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya amependekeza kuwa, umoja huo unapaswa kusitisha mazungumzo yake ya kisiasa na Israel kutokana na utawala huo kuendelea kufanya mauaji na jinai huko Gaza na Lebanon.
Afisa huyo mwandamizi wa Umoja wa Ulaya ameashiria “wasiwasi mkubwa kuhusu ukiukwaji wa sheria za kimataifa na haki za binadamu huko Gaza” na kueleza kwamba “Israel haijashughulikia vya kutosha wasiwasi huu.”
Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya amesema kuuwa, kuna haja ya kutumiwa njia nyingine kama ya kusitishwa mazungumzo ya kisiasa ya Umoja wa Ulaya na utawala wa Israel kama moja ya hatua za kuufanya utawala huo uheshimu kanuni na sheria za kimataifa.
Hayo yanaripotiwa katika hali ambayo, Ofisi ya Vyombo vya Habari vya Serikali ya Ukanda wa Gaza huko Palestina imetangaza kuwa, wanajeshi makatili wa Israel wameua shahidi zaidi ya raia 2,000 kaskazini mwa ukanda huo baada ya utawala huo ghasibu kuanzisha kampeni ya kuangamiza kabisa kila kitu cha eneo hilo tangu siku 38 zilizopita.