Borrell ataka kutekelezwa uamuzi wa mahakama ya ICC dhidi ya Netanyahu na Gallant

Kamishna wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya, Josep Borrell, ametoa wito wa kutekelezwa uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) dhidi ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, na waziri wake wa zamani wa vita, Yoav Galant.

Borrell ambaye alikuwa akizungumza jana, Jumanne, kando ya mkutano wa G7 karibu na Roma, alieleza kuwa nchi za Ulaya zitatekeleza wajibu wao kuhusu Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu na vilevile uamuzi wa mahakama hiyo dhidi ya Netanyahu na Gallant.

Ameongeza kuwa: “Haiwezekani kuikubali Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu inapokuwa dhidi ya Putin, na kuipinga inapokuwa dhidi ya Netanyahu.”

Itakumbukwa kuwa, Tarehe 22 Novemba, Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) ilitoa hati ya kukamatwa Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, na aliyekuwa waziri wa vita wa utawala huo, Yoav Gallant, kwa tuhuma za kufanya uhalifu wa kivita na jinai dhidi ya binadamu huko Gaza.

Kuhusu makubaliano ya kusitisha mapigano nchini Lebanon, Borrell amesema kuwa Israel haina kisingizio cha kukataa makubaliano hayo, kwa sababu yanatoa dhamana zote muhimu za usalama kwa ajili ya utawala huo.

Kamishna wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya amedokeza kuwa nyumba laki moja zimeharibiwa kwa mashambulizi ya Israel nchini Lebanon, na lazima kutolewe mashinikizo dhidi ya Israel ili ikubali pendekezo la kusitisha mapigano.