
Dar es Salaam. Meya wa zamani wa Kinondoni na Ubungo, Dar es Salaam, Boniface Jacob ataendelea kubaki mahabusu, huku hatima ya dhamana yake ikitarajiwa kutolewa Oktoba mosi, 2024.
Jacob, maarufu Boni Yai, mkazi wa Mbezi Msakuzi anakabiliwa na kesi ya uchapishaji taarifa za uongo kwenye mitandao, ambayo upelelezi wake haujakamilika.
Kutokana na kesi hiyo, upande wa mashtaka uliwasilisha maombi mawili, ukiomba Mahakama iamuru atoe nywila (neno la siri) za simu zake na akaunti yake ya mtandao wake wa X (zamani twitter), ili vifanyiwe uchunguzi na mpelelezi.
Pia uliomba Mahakama izue dhamana yake kwa madai ni kwa usalama wake, ukidai maombi hayo yanatokana na kile mshtakiwa alichomweleza Mkuu wa Upelelezi Mkoa (RCO) wa Kinondoni, Davis Msangi kuwa baada ya taarifa alizoandika anajua kuwa atatekwa na kuuawa.
Maombi hayo yalipingwa na jopo la mawakili wa Boni Yai lililoongozwa na Peter Kibatala, wakidai hoja hizo hazina mashiko na kwamba maombi hayo hayakuwasilishwa kwa mujibu matakwa ya kisheria.
Waliiomba Mahakama iyatupilie mbali na badala yake impe masharti ya dhamana mshtakiwa, wakidai dhamana ni haki ya msingi ya kikatiba na suala la usalama si moja ya mambo yanayoweza kusababisha mshtakiwa anyimwe dhamana.
Maombi ya upande wa mashtaka yalitarajiwa kuamuriwa leo Septemba 26, 2024 na Hakimu Mfawidhi Franco Kiswaga anayesikiliza kesi hiyo.
Hata hivyo, uamuzi huo ambao ungetoa hatima ya dhamana yake haukutolewa, baada ya upande wa mashtaka kuibuka na maombi mapya yaliyozua mvutano yakipingwa na mawakili wa Boni Yai.
Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Job Mrema wameiomba Mahakama waondoe ombi la amri ya Mahakama kwa mshtakiwa kutoa nywila zake, wakidai waliwasilisha kimakosa kinyume cha sheria.
Kibatala, akisaidiana na John Mallya na Michael Luhona licha ya kupinga, Mahakama imekubaliana na upande wa mashtaka na kuliondoa mahakamani ombi hilo.
Baada ya hilo, mawakili wa Serikali wameomba kuwasilisha kiapo cha ziada, ombi lililopingwa na kina Kibatala wakidai halijafuata matakwa ya kisheria na kwamba katika hatua iliyofikiwa ya Mahakama kutoa uamuzi haikubaliki kuwasilishwa kiapo cha ziada ambacho ni ushahidi mwingine.
Kutokana na maombi mapya, Mahakama imeshindwa kutoa uamuzi uliokuwa imeuandaa kuhusu maombi ya awali.
Badala yake, Hakimu Kiswaga ameahirisha kesi hiyo mpaka Oktoba mosi kwa ajili ya uamuzi wa ombi jipya la Serikali kuhusu kuwasilisha kiapo cha ziada.
Kiswaga ameelekeza mawakili wa Boni Yai kuwasilisha kiapo kinzani dhidi ya ombi jipya la upande wa mashtaka.
Kwa mujibu wa Lugina, iwapo Mahakama katika uamuzi wa Oktoba mosi itakubaliana na maombi ya Serikali kuwasilisha kiapo cha ziada, maombi ya awali ya kuzuia dhamana yaliyotarajiwa kutolewa uamuzi yatasikilizwa upya.
Boni Yai alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Septemba 19, 2024 na kusomewa mashtaka mawili aliyoyakana.
Mashtaka hayo ni kuchapisha taarifa za uongo katika mfumo wa kompyuta katika akaunti ya X yenye jina la Boniface Jacob @Ex MayorUbungo kwa nia ya kupotosha umma, kinyume cha kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Kimtandano namba 14 ya mwaka 2015.
Anadaiwa Septemba 12, 2024 jijini Dar es Salaam alichapisha taarifa za uongo zikimhusisha Mkuu wa Upelelezi wa Kanda (ZCO) ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP).
Pia anadaiwa Septemba 14, 2024 jijini Dar es Salaam alichapisha taarifa za uongo zinazowahusisha wakuu wa upelelezi wa mikoa na utekaji na mauaji ya watu na kutupa miili yao.