Bomoa bomoa nyingine yaja, maeneo 111 kupangwa upya

Dodoma. Maeneo 111 katika mikoa 24 yenye makazi duni na yanayoendelezwa kiholela nchini, yanaanza kufanyiwa maboresho kupitia upangaji upya wa miji, huku Serikali ikiahidi kushirikisha wananchi kwa karibu katika mchakato huo.

Hatua hiyo inatekelezwa chini ya Programu ya Uendelezaji wa Miji, inayoendeshwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Marekebisho hayo yanachochewa na ongezeko la idadi ya watu, kupungua kwa ardhi inayomilikiwa binafsi, upanuzi holela wa miji, ukosefu wa nyumba bora na za gharama nafuu, pamoja na lengo la kupunguza gharama za maisha.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na Mwananchi hivi karibuni, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Deogratius Ndejembi amesema programu hiyo inahusisha kuboresha na kurejesha maeneo ya miji ambayo yameathiriwa na changamoto mbalimbali.

Amezitaja changamoto hizo ni pamoja na ukosefu wa huduma za msingi, miundombinu, makazi duni au chakavu, ukosefu wa mifumo ya maji taka na uwepo wa tatizo la uzagaaji wa taka ngumu zinazosababisha uchafuzi wa mazingira.

Ndejembi amesema kutokana na hilo, Serikali sasa inakwenda kuyapanga maeneo 111 katika mikoa 24 yenye ukubwa wa hekari 24,309.349.

Ameyataja maeneo ya kipaumbele kwa sasa ni la Makangira katika Kata ya Msasani, Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam na Maanga lililopo Kata ya Maanga jijini Mbeya na tayari hatua za awali zimeshaanza kuchukuliwa.

Akizungumzia eneo la Makangira linalokusudiwa kuendelezwa upya Waziri Ndejembi amesema lina ukubwa wa hekari 17.72 na wakazi 5,247 kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 huku idadi ya kaya zikiwa ni 1,000.

Kwa upande wa Maanga Mkoa wa Mbeya, Ndejembi amesema eneo hilo lina ukubwa wa hekari 43.6 yenye jumla ya watu 10,047 na kaya 2009.

“Programu hii inatarajiwa kuwa shirikishi kwa kiwango kikubwa ikilenga wananchi wanaoishi katika maeneo hayo kuwa wanufaika wa kwanza, baada ya kuboreshwa kwa eneo husika na uendelezwaji upya wa makazi kufanyika,” amesema.

Unaanza lini

Ni lini kazi hiyo inaanza, Waziri Ndejembi amesema hatua za awali za utekelezaji wa mradi huo zimeanza kwa mwaka huu wa fedha 2024/25 katika eneo la Makangira na Maanga kwa kubainisha eneo la mradi na mazungumzo ya awali ya kujenga uelewa kwa wananchi katika maeneo ya mradi.

Pia, amesema nadharia mbalimbali za uendelezaji upya wa maeneo hayo imefanyika.

Amesema utekelezaji wa mradi wa uendelezaji upya eneo la Makangira Msasani jijini Dar es Salaam unakadiriwa kugharimu Sh230 bilioni huku Maanga jijini Mbeya ukikadiriwa kugharimu Sh440 bilioni.

“Miradi hii itaendelea kutekelezwa kupitia Mradi wa Kupanga kupima na kumilikisha ardhi kwa fedha kutoka serikalini kupitia mradi wa uendelezaji upya wa maeneo kongwe,” amesema Ndejembi ambaye pia ni Mbunge wa Chamwino.

Amesema katika mwaka wa fedha 2024/25, Sh116 milioni zilitengwa kwa ajili ya kuwezesha maandalizi ya uendelezaji upya wa maeneo kongwe.

Amesema lengo kuu la programu hiyo ni kuboresha maisha ya wakazi, kupunguza umaskini, kuongeza fursa za kiuchumi na kuhakikisha miji inakuwa endelevu na inayoweza kukabiliana na changamoto za siku zijazo za kimaendeleo na mabadiliko ya tabia nchi kwa kuwa na majengo, miundombinu na huduma zinazoweza kuhimili changamoto hizo.

Haki za wamiliki

Ndejembi amesema utekelezwaji wa mradi wa uendelezaji upya maeneo chakavu na kongwe miji utafanyika kwa kuzingatia dhana ya kukusanya ardhi na kuipanga upya (Land pooling or Land readjustment).

“Uzoefu wa utekelezaji wa dhana hii duniani kote inahusisha jamii kwa kiwango kikubwa na kufanya uchambuzi wa hali ya kijamii na kiuchumi ya kila mmiliki wa ardhi na nyumba katika eneo la mradi kabla ya kuanza kwa utekelezwaji wa mradi,” amesema.

Waziri huyo ameiambia Mwananchi kuwa kazi hiyo ni muhimu kwa ajili ya kutambua haki na wajibu wa kila mmiliki ndani ya mradi pamoja na kupendekeza mbinu bora za utekelezaji wake. Amesema hiyo inajumuisha upatikanaji wa makazi katika mradi mpya na kubaini idadi ya wakazi wa awali watakaohitajika kuhama ili kuruhusu kuanza kwa utekelezaji wa mradi.

Ndejembi amesema katika utekelezaji wa mradi huo, gharama za pango la nyumba kwa wananchi wote watakaohitajika kuhama kwa muda, zitalipwa na mradi.

“Hii itahakikisha kuwa wakati ujenzi wa makazi mapya ya watu wengi ukiendelea, wakazi wa eneo husika watakuwa na sehemu ya kuishi hadi watakapohamishiwa kwenye nyumba hizo mpya,” amesema waziri huyo.

Amesema kila kaya itakayobainishwa kwenye eneo la mradi itakuwa na haki ya kupata nyumba katika eneo la mradi kwa kuzingatia hali ya makazi yake ya awali na thamani ya gharama ya makazi yake na makazi mapya yatakayoboreshwa.

Amesema Serikali imedhamiria kuboresha makazi ya wananchi na hakuna mwananchi atakayehamishwa moja kwa moja katika eneo la mradi, labda kwa ridhaa yake mwenyewe.

Sababu za mradi

Akizungumzia mradi huo, Waziri Ndejembi amesema kumekuwa na ongezeko kubwa la watu nchini kutoka milioni 12.3 mwaka 1967 hadi milioni 61.7 mwaka 2022 na kwa  mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022, maoteo ya idadi ya watu nchini kwa mwaka 2050 yanatarajiwa kufikia milioni 114.46.

Amesema kwa mujibu wa sensa hiyo, kati ya watu wote, asilimia 68.4 wataishi mijini sawa na watu milioni 78.29.

Amefafanua kuwa hivi sasa idadi ya watu wanaoishi mijini kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi 2022 ni asilimia 34.9.

“Kasi ya kupungua kwa uwiano wa ardhi inayomilikiwa na mtu mmoja mmoja (Land share per capita) kutoka hekari 7.2, mwaka 1978, uwiano huu ulipungua hadi wastani wa hekari 1.44 kwa mtu mwaka 2022,”amesema.

Ndejembi amesema upatikanaji wa viwanja vipya maeneo mapya ya miji hautakuwa endelevu tena ifikapo mwaka 2050, isipokuwa kwa kupanua mipaka ya miji kuvamia maeneo ya kilimo vijijini na maeneo ya hifadhi hali itakayoathiri usalama wa chakula na baioanowi muhimu kwa Taifa. 

Pia, amesema takwimu za Sensa ya Taifa ya Majengo ya Mwaka 2022 imebainisha kuwa asilimia 67.1 ya majengo yote nchini yapo katika maeneo ambayo yameendelezwa kiholela.

“Takwimu hizi zimeonesha umuhimu wa kuja na mikakati madhubuti ya kuboresha makazi yao ambayo kimsingi yamechukua sehemu kubwa ya majengo nchini,”amesema.

Amesema kutokana na hayo wizara ilibaini kupitia tafiti mbalimbali kuwa programu ya uendelezaji upya wa miji itawezesha miji ya Tanzania kuwa himilivu, kuongeza uwekezaji, kuinua uchumi wa Taifa, kujali na kuboresha maisha na mazingira wanayoishi jamii ya Kitanzania.

Faida za programu hiyo

Ndejembi amezitaja faida ni kuwezesha upatikanaji wa ardhi iliyopangwa kwa matumizi mbalimbali ambayo ni kichocheo cha ongezeko la shughuli za kiuchumi na kijamii.

Ametaja faida nyingine ni kuwezesha upatikanaji wa nyumba hususan za makazi na biashara, hatua itakayosaidia kutatua changamoto ya makazi duni katika maeneo ya miji nchini.

“Kuwezesha kutenga maeneo yatakayotumika kama vituo (hubs) tegemezi vya kibiashara au utoaji huduma mbadala na kuchochea ongezeko la shughuli za utalii hususan kwenye miji mikongwe iliyohifadhiwa na kupangwa upya,” amesema.

Faida nyingine ni kuongeza wigo wa mapato ya Serikali kutokana na uwekezaji utakaofanyika na makusanyo yatokanayo na pango la ardhi na majengo ambayo kwa sasa katika maeneo hayo hazikusanywi.

Nyingine ni kuongeza usalama wa miliki za wananchi katika maeneo husika kwa kupatiwa hati za sehemu ya jengo na kuwawezesha wananchi kiuchumi kwa kugeuza ardhi mfu kuwa na thamani.

Kwa upande wa hasara za ujenzi holela, Ndejembi amesema ni hatari kwa usalama wa majengo, mandhari ya mazingira, migogoro ya ardhi, ukosefu wa huduma za jamii, athari za kiuchumi, usalama wa milki, uhamiaji duni na kukosa mipango endelevu.

Kuhusu udhibiti wa ujenzi holela, Ndejembi amesema kinachofanyika ni kuimarisha mipango miji, kusimamia sheria kikamilifu, kuongeza elimu kwa wananchi, kutenga raslimali za fedha, ushirikiano kati ya Serikali na wananchi, matumizi ya teknolojia katika upangaji wa ardhi.

Ameshauri wananchi kujifunza sheria na taratibu zinazohusiana na ujenzi katika maeneo yao zinazojumuisha kuelewa umuhimu wa vibali vya ujenzi, ambayo ni muhimu kwa ajili ya kuhakikisha kuwa majengo yanajengwa kwa viwango vinavyotakiwa na katika maeneo salama.

“Kutozingatia sheria hizi kunaweza kusababisha madhara makubwa kama vile kuanguka kwa nyumba au mafuriko, kupoteza mali kwa kuvunjiwa jengo au vifo kutokana na kuanguka kwa jengo,” amesema Waziri Ndejembi.

Akilizungumzia hilo, kiongozi mmoja wa eneo la Maanga jijini Mbeya, aliyeomba hifadhi ya jina lake kwa kuwa si msemaji, amesema anafahamu kuwapo mpango huo, lakini hana taarifa zozote alizopewa kwa utekelezaji.

Amesema alisikia kuwapo mpango huo, maarufu mpango kabambe katika kata tofauti za jiji hilo lakini huenda bado upo chini ya halmashauri.

“Nilisikia ni maeneo matatu, Maanga, Sinde na Ruanda lakini kwa kuwa halijatufikia huku chini tunasubiri utaratibu zaidi.” amesemakiongozi huyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *