Bodi ya Mikopo Elimu ya Juu kukusanya Sh200 bilioni kwa wanufaika

Unguja. Wakati Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) imetimiza miaka 20, imeendelea kuonyesha mafanikio katika sekta ya elimu ya juu nchini, ikikusanya fedha kwa kiwango kikubwa ili kusaidia wanafunzi kupata mikopo ya masomo.

Mkurugenzi wa HESLB, Dk Bill Kiwia, ameeleza kuwa makusanyo ya mikopo yameongezeka kwa mwaka huu, ambapo wanatarajia kukusanya Sh200 bilioni, ikiwa ni ongezeko kubwa ukilinganisha na mwaka jana ambapo walikuwa wakikusanya wastani wa Sh55 bilioni kwa mwaka.

Akizungumzia maonyesho hayo ya huduma kwa wateja yaliyoanza Februari 11, 2024 katika viwanja vya Kisonge, Unguja, Dk Kiwia alisema mafanikio yamepatikana kupitia uboreshaji wa mifumo na ushirikiano wa karibu kati ya bodi na wadau mbalimbali, hasa waajiri na sekta nyingine za uchumi.

Alisema kuwa katika kipindi cha miaka 20 tangu kuanzishwa kwa bodi hiyo, ni muhimu kuadhimisha mafanikio hayo na kuwahamasisha wanufaika wa mikopo kuendelea kulipa mikopo yao kwa wakati ili faida hiyo iweze kutumika kwa wanafunzi wengine.

Bodi ya Mikopo imekuwa na mchango katika kufanikisha elimu ya juu nchini, ambapo mwaka huu wanatarajia kuwadhamini wanafunzi 247,000. Jumla ya Sh787 bilioni zimetolewa kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi hao.

Katika maonyesho haya, wananchi 45,862 walitembelea maonyesho hayo yaliyofanyika katika miji mbalimbali ya Tanzania, ikiwa ni pamoja na Dar es Salaam, Zanzibar, Arusha, Mtwara, Dodoma, Mbeya na Mwanza. Huku Zanzibar pekee ikiwa na idadi ya watu 5,600 waliotembelea maonyesho hayo.

Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Mikopo Zanzibar, Umrat Suleiman, alieleza kuwa zaidi ya wanafunzi 18,570 kutoka Zanzibar wamefaidika na mikopo, na mpaka sasa wamekusanya Sh24.10 bilioni.

Alisema mikopo imewasaidia wanafunzi wengi kupata fursa ya elimu ya juu na kuendelea kuchangia katika maendeleo ya jamii.

Kwa upande wake Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Lela Muhamed Mussa, alisisitiza kuwa bodi ya mikopo imeonyesha ufanisi katika kutoa mikopo kwa usawa na bila ubaguzi, na inatekeleza dhamira ya Serikali ya kuhakikisha Watanzania wanapata fursa ya elimu bila vikwazo vya kifedha.

Miongoni mwa wanafunzi wanaonufaika na mikopo hii ni Salha Bakari Said, ambaye anasoma katika Chuo Kikuu cha Abdurahman Al Sumait, alisema mikopo hiyo ni muhimu hasa kwa wanafunzi wanaotoka kwenye kaya masikini.

Salha ambaye alipata mkopo kupitia Mpango wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), alisema mpango huu umeleta mabadiliko katika maisha yao.

Alitoa wito kwa Serikali kuendeleza mpango huu kwani unasaidia wanafunzi na pia jamii kwa ujumla.

Mwanafunzi mwingine Aisha Ali Mtumwa, anayesoma kozi ya sayansi ya elimu katika Chuo Kikuu cha Abdurahman Al Sumait, alieleza kwamba familia yake inahitaji msaada zaidi kwa kuwa yeye pekee ndiye amepokea mkopo, ingawa wapo wengine wengi wanahitaji msaada kama huu.

Miraji Alfan Musa, mwanafunzi mwingine anayenufaika na mikopo kupitia TASAF, alionyesha kuwa mpango huu umechangia kupunguza umaskini katika familia yake.

Alieleza kuwa mzazi wake alifanikiwa kuanzisha biashara ya kufuga kuku kwa msaada wa fedha za TASAF, na hata hivyo, anapata msaada wa ziada kutoka kwa fedha za mkopo ili kumudu gharama za maisha.

Alisisitiza kuwa iwapo mpango huu utasitishwa, itakuwa ni changamoto kubwa kwa jamii nyingi, kwani umesaidia kupunguza mzigo wa kifedha kwa kaya maskini.

Mratibu wa TASAF Unguja, Makame Ali Haji alieleza kwamba kuanzia mwaka 2020 hadi sasa, zaidi ya wanafunzi 100 kutoka kaya masikini wamefanikiwa kuingia katika elimu ya juu na kupata mikopo kutoka Bodi ya Mikopo.

Alisema kuwa idadi ya wanafunzi wanaofaidi na mikopo imeongezeka, na aliomba bodi hiyo kuongeza juhudi ili kutoa mikopo kwa asilimia 100 kwa wale ambao bado hawajapata msaada.

Alipongeza bodi ya mikopo kwa kuweka kipengele cha kutambulika kwa wanafunzi kutoka kaya maskini, kwa kutumia namba za mpango wa kaya maskini ili kuhakikisha wanafunzi hawa wanapata mikopo kwa usawa.

Kuanzishwa kwa HESLB

Safari ya kutoa mikopo ilianza mwaka 1992 baada ya kupitishwa kwa sera ya uchangiaji gharama ya elimu ya juu, na mwaka 2004 sheria ilipitishwa na Rais Benjamin Mkapa ili kuanzisha utekelezaji wa mpango huu.

Hadi sasa, jumla ya Sh8.2 trilioni zimetolewa kwa wanafunzi 830,000, na bodi hiyo inaadhimisha miaka 20 ya utekelezaji ambayo ni ishara ya mafanikio makubwa ambayo bodi imeshiriki katika kuboresha elimu ya juu nchini.

HESLB inaendelea kuwa chombo muhimu katika maendeleo ya elimu ya juu nchini.

Inapohitimisha miaka 20 ya utekelezaji wake, mafanikio haya ni matokeo ya juhudi za pamoja za Serikali, bodi, na wadau mbalimbali.

Mikopo hiyo imeweza kuwasaidia maelfu ya wanafunzi kupata elimu ya juu na, hivyo, kuchangia katika maendeleo ya taifa.

Hata hivyo, bado kuna changamoto za kutosha na haja ya kuendelea kuboresha mifumo ili kuhakikisha kuwa zaidi ya wanafunzi wanapata fursa za kielimu, hasa kutoka kwa kaya maskini.