
Dar es Salaam. Wakati uongozi wa Yanga ukiripotiwa kupeleka malalamiko katika Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Michezo (Cas) kudai pointi tatu za mezani za mchezo wao ulioahirishwa dhidi ya Simba, Machi 08 mwaka huu, Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imesema kama uamuzi huo ni kweli utakuwa ni jambo la kuchekesha.
Akizungumza na Mwananchi Digital, mwenyekiti wa TPLB, Steven Mnguto amesema kuwa hilo ni jambo la kushangaza kwa vile linaweza kumalizwa kwa majadiliano ya ndani na mamlaka za soka nchini.
“Cas huwezi kuzungumza tu Cas ni rahisi lakini ina taratibu zake. Lakini kwa sababu wenzetu walishawhai kwenda Cas kwa suala la Cas kwa suala la Morrison sina shaka wanajua hizo taratibu na watazipitia hizo taratibu kwa hiyo kama wanaenda Cas leo huwezi kumkataza mtu kubwa sisi ni kuja kujibu kama tutaitwa na Cas kwenda kujibu na tunayo na wakati huo kama tumeshafanya maamuzi yetu, tutapeleka kwamba maamuzi yetu ni hivi.
“Lakini kama wanaenda Cas sasa hivi ambapo hatujasema kwamba hii imeamriwa vipi itakuwa ni kitu kichekesho. Lakini labda kwa sababu hii ni timu tajiri wanaweza kwenda Cas wakauliza kuna jambo moja mbili tatu utaratibu wake ni nini halafu wakaja kutungojea sisi tufanye maamuzmi nini halafu wakarudi tena Cas lakini sitaki kuamini wanaweza wakafanya hivyo kwa jambo ambalo linaweza kumalizwa hapa,” amesema Mnguto.
Mnguto amesema kuwa pamoja na uwepo wa kanuni na taratibu, uamuzi wa suala hilo unahitaji matumizi ya hekima na busara.
“Piga picha unaishusha Yanga au umeishusha Simba ebu piga picha. Lakini kutokana na tumekiuwa na malezi mabaya tangu huko nyuma, sasa ni tatizo kubwa kurekebisha mambo sasa hivi. We mtoto anakua unamfundisha kuongea matusi sasa kuja kumrekebisha yeye atajua kwamba tangu nimezaliwa najua hili ni neno tu la kawaida uje ulirudishe itakuwa ngumu.
“Wewe unaposema kwamba Simba kagomea tunataka tukuelimishe kwamba kagomea au hajagomea pia tunataka tukuelimishe yanga ana haki ya kudai pointi tatu au hakudai sasa haya ni mambo ambayo huwezi ukaja ukasema hiki au hiki kwa vile yana utaratibu kwa hiyo hivi ni vitu ambavyo tunasema kwamba hekima na busara lazima vitumike.
“Sasa huyo asiyetaka kutumia hekima na busara hayuko tayari kutatua tatizo kusema kweli hayuko tayari kutatua hilo tatizo na nia yake ni kutengeneza taharuki ambayo haitakuwa na maana yoyote. Ebu niambie kwamba zinaombeana hizo timu zishushwe daraja unapata faida gani?,” amesema Mnguto.
Inaripotiwa kwamba miongoni mwa madai ambayo Yanga imepeleka Cas ni ya pointi tatu za mezani za mchezo huo ambao haukuchezwa na pia upendeleo wa mamlaka za soka kwa baadhi ya klabu.