Bodi ya Ithibati ya wanahabari yazinduliwa, majukumu yatajwa

Dar es Salaam. Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari imezinduliwa rasmi ikiwa na jukumu la kusimamia viwango vya kitaaluma kwa waandishi wa habari.

Uzinduzi huo unafanyika takriban miezi minne baada ya wajumbe wa bodi hiyo kuteuliwa, ikiwa ni utekelezaji wa takwa la kisheria chini ya Sheria ya Huduma za Habari Sura ya 229.

Septemba 18, 2024, aliyekuwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa aliwateua wajumbe sita wa bodi hiyo kabla ya sekta hiyo kuhamishiwa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamaganda Kabudi akizungumza katika hafla ua uzinduzi Bodi ya Ithibati ya waandishi wa habari leo Machi 3, 2025.

Wajumbe hao ni  mwenyekiti wa bodi ambaye ni mwandishi mkongwe, Tido Mhando, Thobias Makoba, Mgaya Kingoba, Dk Rose Reuben, Dk Egbert Mkoko na Ladislaus Komanya wakiwa wajumbe huku Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa bodi hiyo ni Patrick Kipangula.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo leo Jumatatu Machi 3, 2025, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamaganda Kabudi amesema bodi hiyo itakuwa na jukumu la kusimamia taaluma ya waandishi wa habari kwa kuhakikisha viwango vya kitaaluma na maadili vinazingatiwa.

Waziri Kabudi ameainisha majukumu ya bodi hiyo kuwa ni kushirikiana na taasisi zinazohusika na masuala ya habari ndani na nje ya nchi, kuweka viwango vya taaluma na mafunzo kwa waandishi wa habari na kutunza orodha ya waandishi waliothibitishwa.

Jukumu lingine alilolitaja ni kusimamia hesabu za fedha, mali na madeni ya bodi sambamba na kutekeleza majukumu mengine kulingana na maelekezo ya waziri.

“Pia, kuandaa mafunzo kwa waandishi wa habari, kutunza orodha ya waandishi wa habari waliothibitishwa, kusimamia hesabu za fedha, mali na madeni ya bodi  na kutekeleza kazi zingine ambazo waziri anaweza kuelekeza,”amesema Waziri Kabudi.

Maoni ya wadau

akizungumza katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile amesema uzinduzi wa bodi hiyo ni hatua muhimu kuelekea kuanzishwa kwa baraza huru la habari Tanzania.

Amesema badala ya waandishi na vyombo vya habari kufikishwa moja kwa moja mahakamani kwa madai ya fidia, mashauri hayo sasa yatapitia kwanza kwenye bodi hiyo.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Grayson Msigwa, amesema bodi hiyo imelenga kuimarisha weledi, maadili na uwajibikaji kwa waandishi wa habari.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamaganda Kabudi, akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Bodi ya Ithibati.

“Katika dunia ya sasa yenye mabadiliko ya kasi ya teknolojia na mawasiliano, vyombo vya habari vina jukumu la kutoa habari sahihi za kina na zinazozingatia masilahi ya Taifa na wananchi,” amesema Msigwa.

Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Wizara ya Mawasiliano, Salome Kessy, amesema bodi hiyo itaweka misingi imara kwa taaluma ya uandishi wa habari, huku Mkurugenzi wa Leseni na Ufuatiliaji wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), John Daffa, akisisitiza umuhimu wa usimamizi wa viwango vya taaluma hiyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Kenneth Simbaya amesema agizo la waziri kwa bodi hiyo kutoa elimu kwa wadau wa habari ni hatua muhimu.

Amesema  baadhi ya waandishi wa habari hujikuta wakikiuka sheria na kanuni kwa kutokuwa na uelewa wa kutosha.

“Sasa hili la elimu ni la muhimu sana, si wote wanaelewa haya mambo, msaada wa kuelimishwa ni jambo la msingi sana likizingatiwa,” amesema Simbaya.

Mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika – Tawi la Tanzania (MISA-TAN), Edwin Soko, amesema kuundwa kwa bodi hiyo ni hatua muhimu kwa sekta ya habari nchini baada ya miaka tisa tangu kupitishwa kwa sheria ya habari.

Amesema ni wazi kuwa waandishi wa habari sasa watatambuliwa rasmi na masilahi yao kusimamiwa ipasavyo.

“Sasa sekta ya habari inapata nguvu zaidi. Ili kuwa mwandishi wa habari, utapaswa kusajiliwa rasmi na tunaamini nchi nyingine za Afrika zitakuja kujifunza kutoka kwetu jinsi tunavyoboresha sekta hii,” amesema Soko.