Bodi: Tutaikata Yanga hela za Gamondi

Wakati maswali mengi yakiibuka juu ya hatma ya kifungo cha aliyekuwa kocha wa Yanga, Miguel Gamondi pamoja na faini aliyotozwa, Bodi ya Ligi Tanzania imetoa ufafanuzi.

Gamondi amefungiwa mechi tatu na kutozwa faini Shilingi 2 milioni kwa kosa la kumsukuma na kumuangusha chini kocha wa viungo wa Singida Black Stars, Sliman Marloene baada ya majibishano yaliyotokea wakati timu hizo zikienda mapumziko kwenye mchezo wa ligi ambao ulipigwa kwenye Uwanja wa Amaan Zanzibar na Yanga kushinda bao 1-0.

Hata hivyo, mashabiki walikuwa na maswali mengi kwa kuwa bodi ilitangaza adhabu hiyo leo muda mchache baada ya Yanga kutoa taarifa ya kuachana na kocha huyo raia wa Argentina, hivyo maswali yalikuwa ni nani ana jukumu la kulipa faini hiyo wakati kocha huyo siyo mwajiriwa tena wa Jangwani?

Akizungumza na Mwananchi, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Almasi Kasongo, alisema adhabu ya kulipa fedha aliyopewa na bodi hiyo italipwa kama ilivyotakiwa na mhusika.

“Mhusika ndiye anayesimamia adhabu yake kwa sababu ina muhusu yeye, kuhusu namna ya kulipwa sisi tunatakiwa kuikata Yanga na wao ndio watamalizana na kocha huyo kama wanamlipia sawa watamdai yeye, lakini adhabu ipo palepale,” alisema na kuongeza;

“Kuhusu adhabu ya kufungiwa ni ya kikanuni, hivyo kuhama nayo itategemea kanuni ya nchi husika anapokwenda, kama inatambua wanaweza kumuambia aendelee nayo japo sina uhakika sana kwani hii ni adhabu ya Ligi Kuu Bara.”