
Dar es Salaam. Licha ya kuwapo kanuni kuzuia watoto chini ya miaka tisa kubebwa kwenye pikipiki, wazazi wameendelea kuvitumia vyombo hivyo vya usafiri kama mbadala wa magari ya shule.
Wakati kanuni zikikataza hilo kutokana na watoto kushindwa kujishikilia vizuri kwenye pikipiki hivyo kuwa hatarini, madaktari wanaeleza athari nyingine za kiafya zinazoweza kuwakabili kwa kutumia usafiri huo.
Mtazamo kisheria
Usafirishaji kwa njia ya pikipiki na bajaji unaongozwa na sheria ndogo au kanuni zilizotungwa na Waziri wa Uchukuzi chini ya Sheria ya Utoaji Leseni za Usafirishaji.
Tangu mwaka 2010 zimekuwa zikitumika kanuni zilizotungwa wakati huo na kutangazwa kwenye Gazeti la Serikali Na. 144 la mwaka 2010. Kanuni hizo zilifanyiwa marekebisho mwaka 2017 na kutangazwa kwenye Gazeti la Serikali Na. 419 la mwaka 2017.
Kanuni zinakataza watoto walio na umri chini ya miaka tisa kupanda pikipiki maarufu bodaboda. Kanuni ya 14 (1) inasema mtoto mwenye umri wa miaka tisa au chini ya hapo hataruhusiwa kubebwa kwenye pikipiki.
Kifungu cha pili kinasema mtoto mwenye umri wa miaka tisa au chini ya hapo hataruhusiwa kubebwa kwenye chombo cha miguu mitatu (bajaji) kama abiria, isipokuwa awe ameambatana na mtu mzima.
Madhara ya kiafya
Mbali na madhara ya kimwili, Daktari bingwa wa watoto, Ezekiel Mwita amesema watoto wanaotumia usafiri wa pikipiki wapo kwenye hatari kubwa ya kupata magonjwa ya mapafu kutokana na kuvuta moshi wa injini na vumbi barabarani.
Amesema moshi unaotokana na pikipiki una gesi zenye madhara kama monoksaidi ya kaboni, dioksidi ya salfa na oksidi za nitrojeni, ambazo zinaweza kusababisha matatizo ya kupumua kwa watoto.
“Watoto wanapovuta moshi huu mara kwa mara, njia zao za hewa zinaweza kuvimba na kuathiri ukuaji wa mapafu yao, hali inayoongeza hatari ya pumu na maambukizi ya mapafu kama nimonia,” amesema.
Dk Mwita amesema watoto pia huathiriwa na vumbi la barabarani linaloweza kuingia kwenye mfumo wa upumuaji na kusababisha kikohozi cha mara kwa mara, muwasho wa koo na kupunguza kinga ya mwili dhidi ya maambukizi ya bakteria na virusi.
Hivyo, anashauri wazazi kuhakikisha watoto wanavaa barakoa au kofia ngumu yenye glasi wanapopanda pikipiki ili kupunguza athari za moshi na vumbi.
Amesema uchafuzi wa hewa unachangia kwa kiasi kikubwa magonjwa ya mfumo wa upumuaji kwa watoto duniani, hivyo wazazi wanatakiwa kuwa waangalifu.
Kwa upande wa madhara ya kimwili, daktari wa watoto katika Hospitali ya St Bernard, Lucy Msemwa anasema kuna hatari ya watoto kupata majeraha kichwani kwa sababu ya kutokuwa na kofia ngumu ya kumkinga inapotokea ajali.
Anasema mtikisiko wa pikipiki unaweza kuwa chanzo cha mtoto kupata tatizo la utindio wa ubongo au majeraha ndani ya ubongo, ambayo hayaonekani mara moja.
“Kwa kuwa mwili wa mtoto bado unakua, mifupa yake si imara kama ya mtu mzima. Mtoto anayepandishwa nyuma ya pikipiki yupo hatarini kupata majeraha na kupona kwake inachukua muda mrefu au kumsababishia ulemavu wa kudumu,” amesema.
Ameeleza ni rahisi mtoto kupata tatizo la mgongo na shingo ajali inapotokea au pikipiki inaporuka mashimo barabarani, tofauti na mtu mzima ambaye mifupa yake imekomaa.
Pia anaeleza watoto wamekuwa wakipata majeraha ya moto yanayosababishwa na bomba la moshi lililo pembeni mwa pikipiki (exhaust pipe)
“Nilishamtibu mtoto ambaye ameunguzwa na bomba la kutolea moshi baada ya kuanguka na kulaliwa kwenye mguu, kwa hali hiyo anatengenezewa kovu la kudumu, akiwa mkubwa analaumu aliyempakiza pikipiki,” amesema.
Madhara mengine anasema pikipiki ni chanzo cha watoto kukatwa miguu kutokana na ajali, hivyo kupata ulemavu wa kudumu, huku wengine wakivunjika viungo vikiwamo mikono au miguu.
Kumbukumbu isiyofutika
Nassoro Hussein, mkazi wa Temeke Mikoroshini anasema hataruhusu katika maisha yake kumpakia mtoto kwenye bodaboda.
“Mimi ni dereva wa pikipiki, mwaka 2018 nilitoka nyumba na mtoto wangu wa miaka miwili nikamweka mbele kwenda naye barabarani kununua nyama, wakati naikaribia barabara ya lami niliingia kwenye kishimo mtoto akaanguka.
“Alianguka kwa sababu nilishindwa kumshika vizuri, kwani nilitumia mkono mmoja kumshika na mwingine nilishika pikipiki, hivyo mtoto akafikia kichwa,” anasimulia.
Anasema alimuokota na kumpeleka Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Temeke ambako baada ya madaktari kumpima walimwambia damu imevilia kwenye ubongo na uhakika wa kupona ni mdogo.
Hussein anasema baada ya siku tatu mtoto alifariki dunia. Kifo cha mwanaye, anasema kilimpa msongo wa mawazo akijilaumu kwamba ni muuaji.
“Sikuendesha pikipiki tena, nikaenda kuomba kazi viwandani Barabara ya Mbozi hadi leo nipo huku na sijaruhusu watoto wangu kupanda pikipiki kwa sababu ya kusababisha kifo cha mwanangu,” anasema.
Hata hivyo, Zainabu Salmin, mkazi wa Buguruni Mnyamani amesema usumbufu wa daladala asubuhi ni sababu ya kumpakiza mtoto wake kwenye pikipiki.
“Mara nyingi ninalazimika kumpakia mwanangu kwenye bodaboda kwenda shule kwa sababu usafiri wa daladala ni mgumu asubuhi. Sikujua kama sheria inakataza, ila ninachofahamu ni kuzingatia kumvalisha kofia,” amesema.
Mazingira ya Zainab, hayana tofauti na ya Patrick Shirima, mkazi wa Tabata Kimanga anayesema anatumia bodaboda kwa safari ya mtoto wake shuleni kwa sababu ya kutokuwa na nafasi ya kumpeleka.
“Naondoka saa 11:00 alfajiri kupambana na maisha na nyumbani naishi na mtoto wangu pekee, nimeamua kuchagua mtu mmoja wa kumpeleka shule na kumrudisha nyumbani,” amesema.
Anthony Shaban, dereva wa bodaboda eneo la Magomeni, amesema madereva wengi huwapakia watoto wadogo kwa maombi ya wazazi.
“Mteja akinilipa na kuniomba nimpeleke mtoto wake, siwezi kumkataa. Wengi hata hawajui kama tunavunja sheria na wamekuwa wakitubembeleza na kama wanakaa mtaa mmoja wanachanga tuwabebe kwa pamoja,” amesema.
Amesema wapo wazazi ambao hawajui kama watoto wao wanapandishwa mshikaki, jambo ambalo hufanyika kuepuka gharama ya kurudi eneo la shule mara kadhaa.
Mwenyekiti wa Chama cha Waendesha Bodaboda Dar es Salaam, Charles Massawe amesema wamekuwa wakikazia elimu kwa madereva juu ya sheria zilizopo.
“Elimu tumekuwa tukiisisitiza hata kwenye vikao vyetu vya chama na tumethubutu kwenda kwenye nyumba za ibada kutoa elimu kwa wazazi wanaotumia bodaboda,” amesema.
Anasema licha ya elimu kutolewa, hali ya maisha inachangia watoto kuwekwa kwenye hatari kwa kupandishwa kwenye pikipiki.
“Sheria zipo wazi na sisi hatubariki kabisa kwenye kupakia watoto chini ya miaka tisa kwenye pikipiki, na tumetoa ruhusa kwenye vijiwe ikiwezekana anayekiuka sheria afukuzwe,” amesema.
“Hatuna kofia ngumu, watoto tunaowabeba wanachoka na kulala wakiwa njiani na hawawezi kujishikilia, lakini sisi tunakomaa kwa kuhofia kuvunja ujirani, inabidi kuwa wawazi sasa,” amesema.
Massawe ametoa wito kwa wazazi na walezi kuona thamani ya watoto wao isije kuonekana elimu anayopigania kwa kijana wake ikawa bure na baadeye kupokea lawama ya kuwa chanzo cha ulemavu au kifo cha mtoto.
Usimamizi wa sheria
Akizungumza na Mwananchi Februari 26, 2025 Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Solomon Mwangamilo alisema wamekuwa wakitoa elimu shuleni na kuomba kwenye vikao vya shule waitwe.
Alisema hatua hiyo imechukuliwa kwa kuwa usafiri huo unatumika kwa wanafunzi zaidi, huku wazazi wakiwapandisha watoto kwenye pikipiki moja zaidi ya wanne.
“Hili ni tatizo kubwa kwa sasa na katika kusaidia kulitatua tunatoa elimu kwa wahusika na tunaomba kushirikishwa kwenye vikao vya wazazi na walimu lakini changamoto iliyopo wazazi hawatokei,” amesema.
Amesema Sheria ya Usalama Barabarani ya mwaka 1973 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2022 haielezi kuhusu usafiri wa bodaboda bali wanatumia kanuni za usafirishaji za mwaka 2010.
Amesema uelewa kwa wazazi ni mdogo kwa kukubali kutoa gharama ndogo bila kujali usalama wa mtoto wake na wakati mwingine analazimika kugharimia pakubwa matibabu baada ya tatizo kujitokeza.
Licha ya mtazamo huo wa polisi, Wakili Sosteness Sanga amesema vyombo vya usalama barabarani vinapaswa kusimamia kikamilifu utekelezaji wa sheria na kuchukua hatua stahiki dhidi ya wale wanaokiuka.
“Kwa uchache wao wanatakiwa kujipanga ili kusimamia hili maana hawawezi kukwepa lawama, akishauri kuanzisha kitengo maalumu kitakachokuwa kinashughulikia pikipiki tu huku na wao wakiingia barabarani kuangalia hali iliyopo,” amesema.
Mdau wa usalama barabarani, Ramadhan Nassor amesema wazazi wanatakiwa kutafakari athari ya matumizi ya chombo cha moto kwa watoto wao.
“Kuna haja ya kuwa na kampeni endelevu ya kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa kufuata sheria za usalama barabarani kwani matumizi ya bodaboda kwa watoto yanaongezeka kila uchao,” amesema.