Bodaboda, bajaji wanavyopiga hela kwa kutumwa kondomu

Dodoma. Aibu kwa watumiaji wa kondomu imewalazimu kuwalipa madereva wa bodaboda na bajaji kwenda kuwanunulia kinga hiyo dhidi ya magonjwa ya ngono na homa ya ini.

Hayo yamebainishwa leo Novemba 19, 2024 katika mkutano wa mwaka wa wadau wa programu jumuishi ya kondomu, uliokuwa ukijadili vikwazo vya matumizi ya kinga hiyo kwa vijana.

Akizungumza suala hilo, Ezra Dyanko dereva wa bodaboda mkoani Dodoma, amesema watu wengi wanaogopa kwenda kuchukua kondomu, hivyo wanawatuma wao kuwachukulia.

“Kama nauli ya kwenda kuzifuata yuko radhi kukuongeza Sh1, 000 au Sh2, 000 kwa ajili ya kwenda kuchukua kondomu, anakwambia ‘bwana mimi naogopa kwenda kuchukua kule zinakopatikana au kuuzwa’.

“Kwa mfano, kuna mtu alinikuta Amani (hospitali) akaniambia ‘nitakupa hata buku mbili (Sh2, 000), wewe nenda kanichukulie, mimi nikienda wataniona wale akinamama’,” ameeleza kijana huyo.

Amesema wamekuwa wakitumwa na wanawake wanaofanya biashara za ngono kwenda kuwanunulia kwa kuwa wateja wao wanahofia kwenda kuchukua bidhaa hiyo katika maduka hadharani.

Amesema utamaduni wa kwenda kuwanunulia kondomu watu umeanza muda mrefu na kuwa hata yeye alikuwa anakwenda kuuza kondomu katika maeneo ya Chako ni Chako kwa wanawake wanaojiuza nyakati za usiku.

“Mwaka juzi muda wa saa 7 usiku nilikuwa nakwenda kuwauzia Chako ni Chako ambapo walikuwa wanatoa hadi Sh1, 500 kwa kila kondomu. Kwa sababu zinakuwa zimewaishia na maduka mengi ukifika muda huo yanakuwa yamefungwa,” amesema.

Amesema dhana iliyopo mtaani hivi sasa ya kuogopa kwenda kuchukua au kununua kondomu, itamalizwa na elimu sahihi juu ya kondomu.

Ofisa Mradi wa Afya Yangu, Steve Mayendeka amesema kumekuwa na mtazamo hasi kuhusu matumizi ya kondomu ikiwa ni pamoja anayezichukua kuonekana anafanya sana ngono.

Kondomu ya kiume yakubalika zadi

Wakati huohuo, Mayendeka amesema kondomu ya kiume imeonekana kukubalika zaidi miongoni mwa jamii kuliko ya kike kutokana na kuwa na watumiaji wengi.

 “Wanaofanya biashara ya ngono, wengi wanagombania kondomu za kiume kwa kuwa ni rahisi kumshawishi mwanaume kuzitumia, kama hataki anaachana nazo. Tutaona kuna changamoto nyingine ya sisi wanaume kuongeza dau katika suala la kutumika kondomu,” amesema.

Amesema kuna maeneo mengine upatikanaji wa kondomu unakuwa ni mgumu akitolea mfano Mkoa wa Singida kwenye maeneo ya uvuvi ambapo akina dada wametengeneza vibanda kwa ajili ya biashara ya ngono.

Mayendeka amesema kutokana na uhaba wa kondomu za bure, inawalazimu kwenda kuzinunua kwa watu wanaozichukua kutoka maeneo mbalimbali, boksi moja wakilinunua kati ya Sh7,500 hadi Sh10,000.

Amesema kuna matumizi yasiyo sahihi kwa wanaume ikiwemo matumizi ya vitu mbadala wa kondomu katika kuzuia maambukizi ya Ukimwi na dhana kuwa usipopata michubuko huwezi kupata maambukizi.

Awali akifungua mkutano huo, Kaimu Meneja wa Mpango Mpya wa Kudhibiti Ukimwi, Magonjwa ya Ngono na Homa ya Inn (NASHCoP), Dk Zeye Masunga amesema kuwa Wizara ya Afya imeagiza kondomu milioni 171 katika kipindi cha kati ya Januari 2023 hadi Oktoba 2024.

Amesema gharama za uagizaji wa kondomu hizo ni Sh14 bilioni. Amesema makasha 58,000 ya kondomu yamesambazwa katika maeneo mbalimbali huku Dar es Salaam ikiwa na mashine tembezi kwa ajili ya huduma hiyo.

Ukosefu wa elimu

Oktoba 24, mwaka jana Gazeti la Mwananchi liliripoti kuhusu uhaba wa elimu ya afya ya uzazi, unaotajwa kuchangia matumizi hafifu ya kondomu.

“Miaka ya 2000 mwanzoni kulikuwa na filamu zilizoonyeshwa vijijini kuhamasisha matumizi ya kondomu, kwenye redio na televisheni pia kulikuwa na matangazo mbalimbali ambayo sasa hayapo,” alisema Amina Ally (52), mkazi wa jijini Dodoma.

Martha Salehe, mwelimishaji rika katika Wilaya ya Ushetu amesema wamekuwa wakiwawaelimisha vijana na hutumia muda wa ziada kufuata kondomu hospitalini na kuwagawia wahitaji bure.

Kwa upande wake, mwelimishaji rika kwa vijana, Godlove Isdory alisema baadhi ya vijana hawatumii kinga na wanapopata magonjwa ya zinaa huishia kwenda kujitibu kwa kununua dawa famasi.

Alishauri vijana wapewe elimu sahihi kuhusu matumizi ya kondomu na kwamba, hilo lisionekane kuwa jambo lililopitwa na wakati.

Mhudumu wa famasi katika stendi kuu ya mabasi jijini Mbeya, Atuganile Ambrose amesema wateja wa kondomu sikui hizi wamepungua.

Alisema awali aliuza pakiti kubwa nne kwa wiki, lakini miaka ya 2019 hadi 2023 anaishia kuuza pakiti moja kwa mwezi mzima.

“Hapa tuna za wanawake pia, lakini zinazouzika zaidi ni za wanaume. Hatuwezi kufanya ulinganifu lakini wateja si wengi kama vile tunavyotarajia,” alisema Emmanuel Shayo, mhudumu wa famasi iliyopo katikati ya jiji la Dodoma.