
Mwanza. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limesema Dereva wa Pikipiki (Bodaboda), Mhochi Herman (29), inadaiwa ameuawa kwa kushambuliwa sehemu mbalimbali za mwili wake baada ya kukutwa na mke wa mtu.
Taarifa ya kuuawa kwa dereva bodaboda huyo imetolewa leo Ijumaa Machi 25, 2025, na Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Wilbrod Mutafungwa ambapo amesema Herman ambaye ni Mkazi wa Kitangiri wilayani Ilemela Mkoa wa Mwanza aliuawa Machi 21, 2025, saa 3:30 asubuhi katika Mtaa wa Ghana, Kata ya Nyamanoro wilayani Ilemela mkoani humo.
Kutokana na mauaji hayo, Polisi mkoani humo inamshikilia Mkazi wa Ghana wilayani Ilemela mkoani humo, Athumani Stanslaus (36) kwa tuhuma za kumuua Herman.
“Athuman baada ya kumfumania Herman akiwa amelala na mke wake alimshambulia kwa kutumia kitu chenye ncha kali sehemu mbalimbali za mwili wake,” alidai Mutafungwa.
Ameongeza kuwa; “Jeshi la Polisi linatoa wito kwa wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi na badala yake watumie njia sahihi wakati wanapopata changamoto za kijamii”
Mbali na tukio hilo, Jeshi hilo linamshikilia Mkazi wa Butonga Wilayani Sengerema mkoani Mwanza, Doto Sanan (18) kwa tuhuma za mauaji ya Eliyas John (18) kwa kumchoma na kitu chenye ncha kali kifuani.
Kwa mujibu wa Kamanda Mutafungwa, alidai tukio hilo lilitokea saa 4:00 usiku Machi 23, 2025, katika Mtaa wa Kome Kata ya Ingurumuki wilayani Sengerema baada ya kuzuka ugomvi baina yao, ambapo mtuhumiwa amehojiwa na upelelezi utakapokamilika hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.