Dar es Salaam. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amesema ni lazima Watanzania wapate huduma bora ya umeme huku akimtaja Rais Samia Suluhu Hassan ametajwa kwa kuwa kinara katika kusukuma kufikiwa kwa malengo hayo.
Dk Biteko amesema azma ya Serikali ni kuhakikisha Tanzania wanapata huduma bora katika sekta mbalimbali za kijamii na kwamba, kwenye umeme kasi ya utekelezaji miradi mikubwa inaendelea.
“Tunamshukuru Rais wetu (Samia Suluhu Hassan) ambaye siku zote anasema wananchi wapate umeme, na naomba nimuahidi kuwa mimi na wenzangu tutafanya kazi kwa kasi unayohitaji ili kuhalikisha wananchi wanapata umeme,” amesema Dk Biteko.

Dk Biteko amesema hayo leo Ijumaa, Mei 2, 2025 wilayani Urambo, mkoani Tabora baada ya kukikagua kituo cha kupokea, kupoza na kusambaza umeme cha Msongo wa Kilovoti 132/33.
Amesema kazi ya kutekeleza mradi huo imefanyika kwa weledi na ametumia fursa hiyo kuupongeza uongozi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kwa kukamilisha mradi kwa ufanisi.
“Mmefanya kazi kwa vitendo, nilikuja hapa mwaka jana mradi ukiwa asilimia 10, maajabu gani mmefanya mmemaliza kazi kwa wakati siwezi kujua. Nataka niwaambie naona fahari kuwa kiongozi wenu, napenda kufanya kazi na watu wenye kuleta matokeo nawashukuru mno,” amesema Dk Biteko.
Pia, ameipongeza Kampuni ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji wa Umeme (ETDCO) kwa usimamizi mzuri wa kituo hicho cha Urambo ambacho kimewashwa kwa siku 20 hadi sasa na kuongeza mapato ya Tanesco kwa asilimia 10.
Ameitaka ETDCO kuendelea kufanya kazi kwa ufanisi na kusema kuwa wanafursa ya kupewa mradi mwingine kwa kuwa wamefanya kazi nzuri.
Amewahakikishia wananchi wa Urambo na Kaliua kuwa wataendelea kupata umeme wa uhakika na mradi huo unaifanya Tabora kuwa chanzo cha umeme katika mikoa ya Katavi na Kigoma.
“Mwishoni mwa mwezi huu (Mei, 2025) tutazima jereta Mpanda na kusaidia wao wapate umeme, watu wa Urambo nataka niwaambie kabla ya kituo hiki kuwashwa makusanyo ya Tanesco yalikuwa Sh323 milioni pekee na baada ya kuwashwa Wilaya ya Urambo Tanesco itapata Sh4.5 bilioni kwa mwaka. Kiuchumi maana yake tumewekeza Sh44 bilioni na hiyo fedha itarudi ndani ya muda mfupi,” ameongeza.
Pia, Dk Biteko amempongeza Mbunge wa Urambo, Margaret Sitta kwa mchango wake na ufuatiliaji wa ujenzi wa mradi wa kituo hicho na kusema kuwa alijitoa kuhakikisha wananchi wake wanapata huduma ya umeme.

Aidha, amesema sekta ya nishati imenufaika na mchango wake na kuielekeza Tanesco kupanda mti na kuupa ukumbi wa mikutano jina la mbunge huyo ikiwa ni sehemu ya kuthamini na kuenzi mchango wake.
Kuhusu Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani unaotarajiwa kufanyika Oktoba 2025, Dk Biteko amewasihi Watanzania kushindana kwa hoja na sera, huku akiwaomba wamuunge mkono Rais Samia kwa nia yake thabiti ya kuwaletea maendeleo wananchi.
Awali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba amesema kufuatia maelekezo na usimamizi makini wa Dk Biteko sasa wananchi wanapata umeme wa uhakika.
“Naibu Waziri Mkuu ni vyema ukafahamu kuwa tangu umeme huu ulivyowashwa haujawahi kuzimika hata mara moja na haya ni matokeo ya usimamizi wako na ninaamini wananchi hawa wa Urambo leo wana haki ya kufurahia uwepo wako,” amesema Mhandisi Mramba.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Renata Ndege amesema mradi huo unakwenda kuufungua mkoa huo na mikoa jirani kwa fursa za kiuchumi na kijamii.
“Mradi huu umekamilika na tumewasha umeme Machi 20, 2025, mahitaji ya umeme kwa Mkoa wa Tabora ni wastani wa megawati 28 sawa na asilimia 32.7 ya uwezo wa vituo vyote ambayo ni megawati 85.5.” amesema Ndege.