
Kahama. Naibu Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko, amewaasa wanachama na viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) katika jimbo la Msalala, wilayani Kahama mkoani Shinyanga, kuungana na kuondoa migogoro iliyopo ndani ya chama hicho ili kuwaletea maendeleo wananchi.
Naibu Waziri Mkuu Dk Biteko ameyasema hayo leo Februari 25, 2025, wakati akihutubia kwenye mkutano mkuu maalum wa CCM jimbo la Msalala, uliolenga kusoma ilani ya utekelezaji ya CCM ya 2020-2025, katika jimbo hilo.
Amewataka wanachama hao pamoja na wananchi kwa ujumla kutatua migogoro baina yao, kusameheana, kupendana na kushikamana kutumia vyema rasilimali zilizopo wilayani humo kwani ni wilaya ya kimkakati, yenye rasilimali nyingi ambazo zikitumika ipasavyo zinaweza kukuza uchumi na kuwaondolea umasikini wananchi wake.
“Viongozi tunaweza kutofautiana hapa na pale kwa msimamo, kwa tafsiri, kwa namna tunavyoona mambo lakini tusifike mbali tukavuana nguo mbele za watu, tukaacha kazi yetu ya kuwaletea maendeleo wananchi” Alisema Dk Biteko
“Tusipotafsiri hali yetu ya kijografia kama wilaya ya Kahama tukaacha kuungana kwa pamoja kama wanaCCM tukashughulika na maendeleo ya watu, tukaanza kushughulikiana wananchi watatushangaa huko wao wanataka maendeleo hawatakimigogoro,” amesisitiza
Naye mbunge wa Msalala, Iddi Kassim ametumia jukwaa hilo kuwaomba radhi watendaji wa halmashauri ya Msalala, wananchi pamoja na wanachama wote wa CCM wa jimbo hilo, na kwamba pale walipotofautiana ni kutokana na harakati za kuwaletea maendeleo wananchi.
“Niwaombe radhi watumishi wa serikali popote ambapo niliwagusa, kwani nilipomgusa mtu yeyote yule wa serikali sikua mimi ilikuwa ni hawa wajumbe ambao walinituma niwaletee maendeleo” Alisema Iddi