
Shirika la Habari la Bloomberg limetangaza kuwa, Mwanamfalme wa Saudia Mohammed bin Salman ameghairi safari yake iliyokuwa imepangwa ya kushiriki mkutano wa kilele wa viongozi wa kundi la mataifa tajiri na yale yanayostawi kiuchumi la G20, unaoanza leo (Jumatatu) huko Rio de Janeiro, Brazil.
Chanzo hicho ambacho kiliomba kutotajwa jina kwenye shirika hilo kutokana na unyeti wa suala hilo, kimedokeza kuwa sababu ya hilo ni kuwa safari ya kwenda Brazil inachukua zaidi ya saa 14, na hivyo huenda ikazidisha tatizo kwenye mfereji wa sikio ambalo mrithi huyo wa kiti cha Ufalme wa Saudia, mwenye umri wa miaka 39, anaugua.
Shirika la Habari la Bloomberg limesema kuwa, afisa wa serikali ya Saudi alikataa kutoa maoni juu ya habari hii baada ya kulizwa kuhusiana na hilo.
Mwanamfalme huyo wa Saudia hapo awali alikumbwa na tatizo la kuziba masikio lililodumu kwa siku kadhaa baada ya safari ndefu za ndege.
Aidha imeelezwa kuwa, mwaka huu Bin Salman alighairi safari za nje katika dakika ya mwisho, ikiwa ni pamoja na ziara rasmi nchini Japan.
Hata hivyo inaelezwa kuwa, kutokuwepo kwa Rais wa Russia Vladimir Putin kwenye mkutano huo na kukaribia mwisho wa muhula wa Rais wa Marekani Joe Biden kunaweza pia kuwa na mchango katika uamuzi wa Mwanamfalme Mohammed bin Salman wa kutoshiriki katika mkutano wa G20.