Dar es Salaam. Mmoja wa wasanii wanaotamba kwa sasa kwenye muziki Afrika ni Bien wa Kundi la SautiSol la Kenya. Moja ya sifa anazopewa kumhusu, ni uwezo wake wa kufanya shoo za jukwaani kwa maana ya ‘live performance’ na kuteka mashabiki waliohudhuria.
Ingawa wasanii wengi wa Tanzania wamekuwa wakifanya shoo hizo, lakini kutokana na uwezo wa Bien, wameonekana wameachwa mbali sana na wanachotakiwa ni kujitahidi kufikia levo yake na kumpita.
Moja ya kauli zilizotolewa kuhusu wasanii wa Bongo kushindwa kufanya shoo za live, ni ya Mtayarishaji mkongwe wa muziki, Master Jay na bila ya kumung’unya maneno na kwa utaalamu wake alisema wazi wasanii wa Tanzania hawana uzoefu na kufanya shoo za jukwaani ‘Live Band’.

Master Jay aliyasema hayo wakati akihojiwa na moja ya vyombo vya habari kabla hata ya usiku wa tuzo za Trace zilizofanyika Zanzibar.
“Mimi naongea kitu cha kweli. Wasanii wetu hawana uzoefu na ‘live band’ siyo kwamba kitu kibaya. Kuna wasanii wanaitwa Studio Musician na kuna wale ambao studio wanaweza na live wanaweza. Siyo kitu kibaya. Imefika sehemu sasa Afrika Mashariki tumeiteka, sasa tunakwendaje mbali zaidi,” alihoji na kuongeza;
“Tunatakiwa kwenda MTV na Grammy. Hatuwezi kwenda huko na watu ambao hawauwezi mziki. Angélique Kidjo (mwanamuziki wa Benin) haimbi kwa Kiingereza lakini ana tuzo kibao za Grammy. Tuzo hazihusu kuwa na wafuasi wengi, mimi nina hasira.”

“Kitu ninachojivunia ni kwamba waburudishaji bora wa Afrika Mashariki wanatoka Tanzania, Wakenya wamebaki na kitu kimoja wanajua Kiingereza na wanatuzidi kuimba, wana waimbaji bora sana.”
Kilichotokea baada ya kauli hiyo
Licha ya kwamba kauli hiyo ilitafsiriwa tofauti na Wabongo, lakini kwenye shoo za usiku wa Tuzo za Trace, ni kama wale waliodhani mtayarishaji huyo wa muziki aliyewatoa wasanii wengi na anayeijua vyema tasnia hiyo anakejeli, watakuwa wamepata majibu.
Ni hivi. Wengi wanadhani Master Jay hawapendi wasanii wa Bongo Fleva na amekuwa akiwasema sana, lakini hawapi maua yao. Hata hivyo, wapo wasanii wanaokubaliana na kauli zake na kutaka wenzao wachukulie kwa namna ya kujenga na si kwamba amewadharau kwani itawasaidia kuendelea kukua kimuziki.

Katika usiku huo wa Trace, kuna baadhi ya wasanii wa Bongo waliimba ‘live’ kama Harmonize, Nandy na Marioo, huku wengine kama Diamond, Zuchu, Jux walifuata midundo ya ngoma zao.
Bien anaweza, somo hili
Katika moja ya shoo za Live za wasanii wa Bongo, ya Marioo aliimba wimbo aliomshirikisha msanii huyo kutoka kundi la SautiSol la Kenya, Bien na kilichotokea ni baada ya msanii huyo kupanda kumsapoti alifanya vizuri na kushangiliwa na wahudhuriaji.
Sio tu kubeba tuzo, alikuwa kama ‘Man of Match’ usiku ule kwani alipafomu vizuri kiasi cha mashabiki kuamsha shangwe ambalo liliokoa jahazi kwa wasanii wa Afrika Mashariki.
Ukiangalia tuzo hizo wala hawakukosea na ndipo ile kauli ya Master Jay inakuja, mziki una vitu vingi, kutoa ngoma nyingi na kuwa na wafuasi wengi siyo muziki, bali kile unachokifanya na kuwaburudisha watu.

Hadi sasa Bien ndie msanii wa kwanza Afrika Mashariki kushinda tuzo ya Grammy kwenye kipengele cha ‘Best Global Music Album’ ambacho alishinda kipitia wimbo alioshikishwa na BurnaBoy ‘Twice As Tall’.
Hii si mara ya kwanza kwa nyota huyo kusifiwa kuimba Live aliwahi kutumbuiza kwenye droo ya makundi ya fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON).
Siyo katika shoo ya usiku huo tu, hata nchini kwao Kenya, amekuwa akifanya shoo kali za ‘live’ na juzi usiku kwenye shoo ya Burna Boy, alipafomu na kundi lake la SautiSol na kusifiwa na msanii Harmonize, akimwita ‘The King Of East Africa’, ingawa mwenyewe alionyesha kukataa jina hilo. Ikimbukwe, ndiye msanii aliyebeba tuzo za Trace kipengele cha ‘Best Artist Eastern Africa’.
Kwenye shoo ya usiku wa Trace, Bien alipafomu ngoma mbili tu alizoshirikishwa na wasanii wenzake, Extra Pressure ya Ben Sol wa nchini kwao Kenya na ile ya Nairobi aliyoshirikishwa na Marioo kwenye albamu ya The Godson.
Lijue kundi la Sauti Sol
Bien-Aimé Baraza ‘Bien’ ni miongoni mwa wasanii wanaounda kundi la muziki wa bendi ya Sauti Sol nchini Kenya. Wengine ni Willis Chimano na Savara Mudigi na mpiga gitaa, Polycarp Otieno.
Sauti Sol ni bendi ya Afropop iliyoanzishwa jijini Nairobi mwaka 2005 na ilianza kama kikundi cha uimbaji wa ‘Acappella’.