Dar/Mikoani. Kupanda na kushuka kwa bei za baadhi ya bidhaa za vyakula nchini kumetajwa kuchangiwa na kumalizika kwa msimu, athari za mvua na maandalizi ya mfungo wa Ramadhani.
Ufuatiliaji uliofanywa na Mwananchi Februari 20, 2025 katika baadhi ya masoko ya mikoa ya Mbeya, Dodoma, Njombe na Dar es Salaam umebaini baadhi ya bidhaa zimepanda bei, huku nyingine zikishuka.
Ongezeko la bei limeshuhudiwa katika bidhaa za mchele, ndizi, maharage, sembe, mahindi, karoti, njegere na vitunguu, huku nyanya na nyama zikishuka katika baadhi ya maeneo.
Hata hivyo, taarifa za Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) zinaonyesha mfumuko wa bei nchini umebakia kuwa asilimia 3.1 tangu Desemba 2024.
Hali ilivyo Dar
Jijini Dar es Salaam, baadhi ya bidhaa zimepanda bei huku nyingine zikishuka ikilinganishwa na Desemba, 2024 na Februari mwaka huu katika masoko ya Kisutu, Tandika, Buguruni, Ilala na Mabibo.

Kisutu bei za rejareja za nyanya zimeshuka hadi kufikia Sh2,000 kwa kilo kutoka Sh2,500 iliyokuwapo Desemba 2025, sababu ikitajwa ni ongezeko la zao hilo sokoni.
“Sisi huwa tunanunua bei ya jumla kwa kilo kwa sababu huwa tunachagua nzuri, kwa sasa kilo tunanunua Sh1,200 ikiwa imeshuka kutoka Sh1,500 hadi Sh1,600 Desemba mwaka jana,” anasema Muhammad Hussein, mfanyabiashara Kisutu.
Katika soko la Sterio Temeke boksi moja la nyanya linauzwa Sh40,000 hadi Sh45,000 kutoka Sh60,000 hadi Sh70,000, bei iliyokuwepo Desemba 2025.

“Mvua ilikuwa kikwazo, sasa imepungua katika baadhi ya maeneo lakini hali hii inaweza kuonekana tena kuanzia mwezi ujao (Machi),” ametahadharisha Rajabu Hussein, mfanyabiashara sokoni hapo.
Mchele katika soko la Kisutu bei imeongezeka ya juu kabisa ikifikia Sh3, 800 na ya chini ikiwa Sh2,500.
“Huu wa Sh3, 800 ulikuwa Sh3,500 na wa Sh2,500 ulikuwa kati ya Sh2,200 hadi Sh2,000. Ongezeko linatokana na watu kuwa na wasiwasi wa mvua inayonyesha katika baadhi ya maeneo ya kilimo,” amesema Jumanne Msuya, mfanyabiashara sokoni Kisutu.
Nyama katika baadhi ya mitaa ya Jiji la Dar es Salaam imeshuka kutoka Sh12, 000 iliyokuwepo Desemba hadi Sh10,000 na Sh9,000, huku wengine wakiendelea na bei ya awali.
Kushuka kwa bei ya nyama kunatajwa kuchangiwa na kushuka bei ya ng’ombe katika mnada wa Pugu.
“Inategemea unachukua wapi, lakini Pugu bei ya ng’ombe imepungua na hii inatufanya tupunguze bei pia,” anasema Emmanuel Chacha, mwenye bucha Mabibo.
Mnadani Pugu bei imeshuka kwa Sh100, 000 kwa ng’ombe kuanzia mwenye kilo 312 na kuendelea hadi wa kilo 72.
Kwa mujibu wa Bodi ya Nyama Tanzania (TMB), ng’ombe wa kilo 312 na kuendelea katika wiki iliyoishia Februari 10, aliuzwa Sh2.6 milioni katika mnada wa Pugu kutoka Sh2.7 milioni wiki iliyotangulia.
Ng’ombe wa kilo 192 na zaidi aliuzwa Sh1.6 milioni kutoka Sh1.7 milioni katika wiki iliyotangulia, huku wa kilo 72 na kuendelea akiuzwa kwa Sh600, 000 kutoka Sh700,000.
Sokoni Buguruni mkungu wa ndizi kutoka Bukoba bei imeshuka kutoka Sh65, 000 hadi Sh45,000 iliyokuwapo Desemba 2024 hadi kati ya Sh35,000 na Sh25,000 kulingana na ukubwa.
Kwenye Soko la Mabibo, gunia la kilo 100 la njegere limepanda bei kutoka kati ya Sh80,000 hadi Sh100,000 Desemba 2024 hadi kati ya Sh160,000 na Sh200,000 Februari 2025.
Kilo ya vitunguu katika masoko ya Ilala, Buguruni na Mabibo ni Sh2, 000 kutoka Sh1,000 hadi Sh1,500 za awali.
Karoti bei ya jumla imepanda kutoka Sh1, 000 kwa kilo Desemba 2024 na sasa ni Sh2,000.
Mkoani Dodoma
Ufuatiliaji wa Mwananchi katika masoko ya Sabasaba, Kibaigwa na Majengo umebaini bei ya kilo moja ya mahindi imepanda kutoka Sh1, 000 Desemba 2024 hadi Sh1,600 kwa baadhi ya maeneo, sababu ikitajwa ni kuadimika kwa bidhaa hiyo wakati mahitaji yakiwa makubwa.

Mfanyabiashara Emmanuel Silayo, amesema mahindi yamepungua sokoni hivyo bei imeongezeka.
“Awali tulikuwa tukinunua kilo moja ya mchele Sh1, 500 kwa bei ya jumla, sasa ni Sh1, 800 hadi Sh2, 000, hivyo ili upate faida ni lazima uongeze pesa kidogo ya usafiri. Unga wa mahindi kilo 25 tunanunua Sh35, 000 kwa bei ya jumla, ndiyo maana kilo ya unga imepanda kutoka Sh1, 000 hadi Sh1,600,” amesema.
Kwa upande wake, Johari Selemani amesema bei ya nyanya, vitunguu, viazi mviringo na karoti zimepanda kutokana na kuadimika.
Sado moja ya nyanya ni Sh5, 500 hadi Sh6, 000 kwa bei ya jumla, hivyo wao hulazimika kuuza rejareja kwa Sh8, 000 hadi Sh10, 000.
Jijini Mbeya
Jijini Mbeya vitunguu vimepanda kutoka Sh30, 000 sasa ni Sh40, 000, mchele umepanda kutoka Sh33, 000 hadi Sh54, 000, wakati maharage yakifikia Sh64, 000, vyote kwa ujazo wa ndoo ya lita 20.

Viazi mviringo vimeshuka bei kutoka Sh16,000 hadi Sh12,000, ndizi zikipanda bei kutoka Sh5,000 kwa mkungu hadi 18,000 na mahindi ndoo ikiuzwa Sh20,000.
Ofisa biashara katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Festo Nashon amesema ili kukabiliana na ongezeko la bei kuelekea mfungo wa Ramadhani ni vyema wakulima wakapeleka bidhaa sokoni badala ya kuuzia shambani, ili kuwezesha soko kupanga bei kulingana na wingi wa bidhaa.
Mkoa wa Njombe
Mkoani Njombe hali ni hivyohivyo, bei ya maharage imeongezeka Sh300 ikilinganisha na Desemba 2024, yakiuzwa Sh3, 000 kwa kilo kutoka Sh2, 700.
Mchele umepanda bei ukiuzwa kati ya Sh2, 000 na Sh3,000 kutoka bei ya awali ambayo kiwango cha juu ilikuwa Sh1,800.

Ofisa biashara katika Halmashauri ya Mji wa Njombe, Mathew Mkongwa anasema ongezeko la bei linatokana na kupungua kwa bidhaa sokoni.
“Awali wazazi walikuwa wakiuza vyakula kwa ajili ya kupeleka watoto shuleni lakini kipindi kama hiki wengi hawapeleki mazao sokoni, hivyo wafayabiashara wanayatafuta kwa kutumia gharama kubwa,” anasema.
Hali ikiwa hivyo sokoni, taarifa zilizotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) zinaonyesha mfumuko wa bei nchini umebakia kuwa asilimia 3.1 tangu Desemba 2024, kiwango ambacho ni chini ikilinganishwa na nchi jirani.
Katika kipindi kama hicho Kenya ilishuhudia ongezeko la mfumuko wa bei kutoka asilimia 3.0 Desemba hadi asilimia 3.3 Januari. Uganda ilipata ongezeko kutoka asilimia 3.3 hadi asilimia 3.6 katika kipindi hicho.
Takwimu hizi zinaifanya Tanzania kuwa nchi inayoongoza katika udhibiti wa mfumuko wa bei ukanda wa Afrika Mashariki lakini pia kiwango cha sasa ni chini ya lengo la kitaifa la asilimia tano.
Kwa mujibu wa mchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Haji Semboja, Tanzania imefaidika kwa kiasi kikubwa na sera thabiti za kiuchumi, hususan katika kudhibiti usambazaji wa fedha sokoni kupitia utekelezaji wa sera madhubuti za kifedha na kiuchumi.
“Kutokana na sera na sheria imara zilizowekwa na taasisi husika za kiserikali pamoja na usimamizi mzuri wa taasisi binafsi, Tanzania imeweza kupunguza shinikizo la mfumuko wa bei,” amesema Profesa Semboja ambaye ni mhadhiri wa uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Kauli za wachumi
Akizungumza na Mwananchi mtaalamu wa uchumi na biashara kutoka UDSM, Profesa Abel Kinyondo amesema utofauti kati ya mfumuko wa bei wa Taifa unaotolewa na Serikali na kile kilichopo mtaani unasababishwa na muda ambao takwimu za mfumuko wa bei zilikusanywa.
Amesema inawezekana wakati takwimu zinakusanywa bei za bidhaa zilikuwa za kawaida ukilinganisha na sasa bei za bidhaa zimeongezeka.
“Zinapotafutwa gharama za mfumuko wa bei zinakusanywa katika kipindi cha muda fulani na siyo kila siku, hivyo inawezekana wakati wanakusanya takwimu bei za bidhaa hazikuwa kama ilivyo sasa,” anaeleza.
Imeandikwa na Aurea Simtowe na Mariam Mbwana (Dar), Rachel Chibwete (Dodoma) Saddam Sadick (Mbeya) na Seif Jumanne (Njombe).